Mwandishi Wetu, Zanzibar
RAIS wa Zanzibar ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dk Ali Mohammed Shein amewataka watumishi wasiotimiza wajibu wao katika katika Baraza la Manispaa ya Zanzibar na halmashauri za miji, wajiondoa wenyewe kabla hajawafukuza.
"Wenye dhamana ya kusafisha mji watekeleze wajibu wao, kama hawawezi waondoke kabla ya mimi liniyewateua sijawafukuza kazi," alisema Dk Shein alipokuwa akizungumza na viongozi na watendaji wa serikali katika kikao cha Majumuisho ya ziara yake katika Mkoa wa Mjini Magharibi, jana.
Alisema mji wa Zanzibar umekithiri kwa uchafu katika kila kona na kwamba hali hiyo inasababishwa na kutowajibika vyema kwa wenye dhamana ya kufanya shughuli za usafi.Alisema kwa kuzingatia hali ilivyo na athari zake, kuna haja kwa watumishi wa Baraza la Manispaa na halmashauri,kubadilika na kuchapakazi kwa bidii.
"Suala la usafi wa mji sina msalie Mtume nitamwajibisha mtu atakayezembea, hatuwezi kuishi katika hali ya namna hii, nakutakeni sasa kuanza kuchukua hatua za kurekebisha mambo,"alisema Dk Shein.
Alisema pale akashuhudia mifugo ikiwa inazagaa ovyo barabarani au mitaani ofisa anayehusika na udhibiti wa mifugo katika maeneo ya mji, atawajibishwa mara moja na kusisitiza kuwa hatakuwa na masihara katika hilo.
Dk Shein alisema SMZ imepata mkopo wa Sh58 bilioni kutoka Benki ya Dunia, kwa ajili ya kuubadilisha mji wa Zanzibar na kuufanya uwe na mandhari inavyovutia zaidi.Kwa mujibu wa rais, mkazo utakuwa katika usafi na utunzaji wa mazingira ya mji huo.
Alisema fedha hizo pia zitatumika katika kugharimia uwekaji wa taa za barabarani, kuboresha barabara za mitaa na ujenzi wa barabara mpya katika baadhi ya mitaa ya Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.
Dk Shein alisema utekelezaji wa mpango huo utanza Julai mwaka huu hivyo na kuitaka jamii kuanza kubadilika.
Akizungumzia sekta ya afya, Dk Shein alisema sekta hiyo inakabiliwa na changamoto kadhaa, lakini serikali itajitahidi kuzipatia ufumbuzi.
Alizitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na upungufu wa vituo vya afya, wataalamu na dawa.Alisema hata hivyo dhamira ya serikali kuipandisha hadhi, Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja ili iwe ya rufaa bado iko pale pale na kwamba suala hilo kwa sasa limo katika mchakato.
Pia alisema kuna haja ya kuanzisha vituo vya afya vya daraja la pili ili kuwawezesha wananchi kupata huduma katika maeneo ya karibu.Kuhusu kilimo, Rais Dk Shein alisema wakulima wanakabiliwa na ukosefu wa mbegu bora na pembejeo jambo linalowafanya wafanya wasifanikiwe zaidi.
Hata hivyo aliwaahidi wakulima kuwa serikali yake, inaendelea na mkakati wa kuwasaidia kupata mbegu bora na mbolea.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment