Na Abdulla Mohammed
WANANCHI wa Zanzibar wamejenga matumaini makubwa na utendaji wa Rais wao Dk.Ali Mohamed Shein, kwa kumchagua na baadae kumsikia na kumuona akiongoza kwa vitendo kwa yale anayosema, hasa kufanya ziara za mara kwa mara kutembelea maeneo ya wananchi na kuona maendeleo yao na changamoto zinazowakabili.
Hata hivyo wasiwasi kwa wananchi hawa unabakia katika changamoto iliyopo ya kufanikiwa dira ‘vision’ njema ya Dk.Shein ya kujenga Zanzibar yenye neema na maendeleo makubwa zaidi, kutokana na ukimya wa muda mrefu wa watendaji wake wakuu Serikalini.
Labda kwa kusikia hilo kupitia vyanzo mbali mbali au kuliona mwenyewe, Dk.Shein amefanya semina elekezi ili kutoa darsa kwa watendaji wa serikali yake, kuanzia Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, Manaibu Katibu Wakuu, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa wilaya na wengine wote walioonekana kuwa na umuhimu wa kupewa somo la uongozi wa pamoja.
Japokuwa yaliyokubaliwa ‘maazimio’ katika semina elekezi hatuyafahamu sisi wananchi, inaweza ikawa si muhimu sana kwetu kuyajua kama ilivyoonekana ila ni vyema waliopewa ambao ni washiriki wa semina hiyo wasiyaache vichwani mwao au kwenye makabati, tunategemea viwe ndiyo vifaa ‘tools’ vya utekelezaji majukumu yao.
Kutokana na kumuona Dk.Shein na wasaidizi wake, Makamu wa Kwanza wa Rais, maalim Seif Sharif Hamad na Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi, wakizunguka maeneo mbali mbali nchini kuona maendeleo na changamoto za wananchi, wengi tunaweza kuamini kuwa lazima watendaji katika semina elekezi wametakiwa kuzidisha kasi ya utekelezaji majukumu yao kwa kuacha kukaa maofisini na badala yake watembelee sekta wanazoziongoza kwa kukutana na wanaowaongoza, pamoja na wananchi Mijini na Vijijini ndio maana vinara wao wanaanza kwa mfano.
Huku tukiendelea kumuona Dk.Shein na wasaidizi wake, maalim Seif na balozi Seif, wakivalia njuga kufuatilia kasi ya maendeleo nchini, tunatarajia pia kuona watendaji nao wakichakarika, badala ya wengi wao kuendelea kufanya kazi kimazowea.
Katika kipindi hicho kifupi kufuatia semina elekezi wananchi wamekuwa wakipata taarifa nyingi za utendaji wa serikali yao, kupitia viongozi hao kwenye vyombo vya habari, jambo ambalo limeongeza imani ya wananchi kwa Serikali kufuatia kutawaliwa na ukimya wa muda mrefu, kiasi wengine kuhoji uwepo wake.
Viongozi hao wakifanya ziara za ndani na nje ya nchi hueleza bayana walichoona na mikakati ya kuiwezesha Zanzibar kufanikiwa kupitia walichojifunza au kuvuna waliposafiri kikazi nje ya nchi, hili linaweza kuwa somo tosha kwa watendaji wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ).
Watendaji wengi wakuu wa SMZ kuanzia Mawaziri hadi Makatibu Wakuu, bado wanaendelea na hulka ya uhafidhina wa kuficha taarifa kwa wananchi na kung’ang’ania hana potofu kuwa safari walizokwenda ni za kazi yao na sio kuwawakilisha wananchi wa Zanzibar.
Tabia kama hii inazusha malalamiko mengi kutoka kwa wananchi na kuibebesha lawama zisizo na msingi serikali, kwani mbali ya kuwanyima haki yao ya msingi kikatiba ya kupata taarifa pia husababisha wanung’unike kwa matumizi ya safari za watendaji bila kujua maudhui na faida zake kwa nchi.
Wale wanaopata fursa kama hii kupitia Serikali ya muungano au kuongozana na viongozi wakuu wa SMZ, wakirejea utadhani waliungana na msafara wa viongozi kiwanja cha ndege na baada ya Rais au Makamu kueleza kwa ufupi kuhusu safari, wao huwa kimya baadae.
Baya zaidi kuna wale wanaoshindwa hata kuwapa taarifa wasaidizi wao kwa utendaji na ufuatiliaji wa makubaliano, hali ambayo mara nyengine huwatia aibu viongozi wetu wakuu wanapokutana tena na ujumbe waliozungumza nao kwa kuulizwa kulikoni, mbona kimya wakati walifikia muafaka.
Kama hiyo haitoshi, watendaji hawa huona na kusikia uwepo wa fursa nyingi ambazo zingeweza kuwasaidia moja kwa moja wananchi wa Zanzibar kupitia vikundi vyao au biashara zao, lakini huubinya bwii, sijui kwa faida ya nani.
Watendaji wetu pia wamekuwa na tatizo la woga dhidi ya vyombo vya habari, ambapo wamekuwa na madai mengi kuwa wanapotoshwa wanapotoa taarifa zao, huku wakisahau kuwa ni wajibu wao kutoa taarifa kwa wananchi kupitia vyombo vya habari.
Watendaji hawa wanapaswa kuelewa kuwa serikali isiyotoa taarifa uwepo wake unakuwa na wasi wasi na pia inapoteza imani kutoka kwa wananchi wake, hivyo wabadilike kuinusuru serikali yetu na chuki kutoka kwa wananchi ilhali inafanya mengi kwa faida ya wananchi wake.
Aidha wafahamu kuwa hata kama kuna maendeleo mengi, changamoto zinazoikabili serikali na wananchi wake zitaendelea kuwepo na kuanikwa na vyombo vya habari, hivyo ukimya wenu haujengi bali zaidi unabomoa.
Msipobadilika watendaji, kutakuja masuala mengi na wananchi kuanza kutiwa sumu dhidi yenu na kuamini kuwa mnaficha madhambi yenu na mtapojaribu kujibu tuhuma hizo mtakuwa mnajipaka kinyesi.
Kama mlivyoagizwa, kinachohitajika ni kufanya kazi kwa ujasiri, umakini na kujiamini zaidi, huku mkiacha kuhofia kujua matatizo ya wananchi mjini na vijijini kwa kuacha kukaa maofisini tu na kutoka nje, kwani tayari mmeshataolewa ukumbi na wakuu wenu.
Kama ambavyo sote tunaelewa kuwa uwajibikaji kwa watendaji wa sekta ya umma Zanzibar ni ‘zero’, jambo hilo kwa kiasi kikubwa linachangiwa na watendaji hawa wakuu kutawaliwa na ubinafsi na kutoelewa vyema majukumu yao kwa umma.
Serikali inapaswa kupongezwa kwa kuweka sheria na kanuni madhubuti makazini kupitia miongozo mbali mbali kama vile ‘GO’, lakini utashangaa na kujiuliza tatizo liko wapi.
Kama hiyo haitoshi serikali imetumia mabilioni ya fedha kuelimisha wataalamu ambapo mamia wamehitimu na wapo nchini kwenye ofisi mbali mbali, nako mafanikio hayapo unapata suala jengine tatizo liko wapi.
Utashangaa unapowasikia wataalamu wetu wakimueleza kiongozi anapokuwa ziarani kwao kuhusiana na mbinu za kufanikisha jambo fulani, ukiangalia utekelezaji katika sekta hiyo utajiuliza kulikoni wakati wataalamu hao wapo hapo mwaka mzima na mishahara wanalipwa kama kawaida.
Wakati umefika wa watendaji wa SMZ kuona aibu, kwani wengine tokea walipopita kwa nusu saa katika taasisi wanazoziongoza kwa kile walichokiita kujitambulisha hawajaonekana hadi laana ya leo.
Hayo majukumu mmepewa kwa kuaminiwa na kutarajiwa kusaidiwa kufikiwa malengo yaliyowekwa, kama hamyawezi jamani si vibaya mkaziarifu mamlaka iliyowateua iwapangie kazi nyengine, badala ya kung’ang’ania mkijua fika hamumudu.
Tukubali kuwa bila watendaji hawa wakuu wa SMZ kubadilika na kuwajibika ipasavyo, si rahisi kufikiwa kwa ‘vision’ nzuri za kiongozi wetu wa kitaifa na ndugu zangu wananchi wanapaswa kuelewa kuwa kila tunapotoa lawama tuzielekeze moja kwa moja kwa mhusika kwa vile tunamjua badala ya kuichanganya serikali nzima, labda atatanabahi na kubadilika.
Eleweni uongozi ni kuwatumikia wananchi kwa faida yao na nchi kwa jumla, tubadilike sasa ili tuweze kujenga Zanzibar iliyojaa neema.
0777 471199
No comments:
Post a Comment