Habari za Punde

BALOZI SEIF AELEZEA UMUHIMU WA UCHAMUNGU

Na Abdalla Ali, OMPR

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameiomba jamii kuongeza ucha Mungu kwa kufanya ibada na kuachana na mambo mabaya yanayoipotosha jamii.

Alisema ucha Mungu ni jibu la matatizo mengi yanayowakabili wanadamu duniani hivi sasa ikiwemo migogoro ya kudhulumiana, ubaguzi na hata kudharauliana.

Balozi Seif aliyasema hayo katika kongamano la kuhamasisha umuhimu wa ibada ya Hijja kwa waisalamu lililofanyika ukumbi wa skuli ya Haile Selassie mjini Unguja.

Alieleza kuwa elimu  ni nyenzo muhimu inayosaidia kuongeza ucha Mungu kwa wanadamu, hivyo aliwataka Masheikh nchini wajitahidi kuwaelimisha waumini na wao wenyewe wajiongezee maarifa ili wawe wepesi wa kufanya ibada kwa ukamilifu na kuwa wasikivu wa kuepukana na mabaya.

Makamu huyo alitoa wito kwa wanaofanya maandalizi ya Hijja kwa jamaa au taasisi husika kufanya maandalizi hayo mapema ili kuwapa muda wa kutosha Mahujaji na wao wa kujiandaa.

Alizitaka taasisi za Hijja zijitahidi kupunguza lawama na shutuma kutoka kwa Mahujaji na wazidishe mipango mizuri ya safari za Hijja ili kuwapunguzia usumbufu waumini.

Naye Katibu Mtendaji wa Wakfu na Mali ya Amana, Sheikh Abdulla Talib Abdulla alizitaka taasisi za Hijja kutoa elimu ya kutosha kwa Mahujaji watarajiwa na kuheshimu mikataba na wateja wao kwa lengo la kuwawezesha kutekeleza vyema ibada ya Hijja bila matatizo

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.