Na Akilimali Maridhawa
Nimesoma kwa furaha sana makala za waandishi mbali mbali wa habari katika magazeti tofauti ndani ya na nje ya visiwa vya Zanzibar juu ya mtazamo wa serikali kuhusiana na suala zima la mashirikiano na waandishi wa Habari.
Nimebaini kuwa baadhi ya waandishi wa habari hawajaridhika na mahusiano yaliyopo baina yao na serikali, hali ambayo inazorotesha utekelezaji wa jukumu lao la kuiunganisha kihabari serikali na wananchi. Maana yangu ni kwamba, kwanza wanatakiwa kufahamu yanayojiri serikalini na nje ya serikali na baadae kutoa taarifa za uhakika na kwa wakati muafaka kwenda kwa jamii na kinyume chake.
Waandishi wamekuwa wakielezea kwa kulaumu usiri mkubwa wa serikali katika utekelezaji wa jambo hili. Wanasema kwa nini serikali imekuwa ikifanya siri hata katika yale mambo ambayo yangepaswa kuwa dhahiri? Nisingependa niwe msemaji wa serikali katika hili, lakini kwa ufahamu wangu mdogo najua kuwa hali ya mahusiano kati ya waandishi na serikali sio mbaya sana kiasi hicho kinachozungumzwa na waandishi, lakini pia kuna sababu nyingi ambazo zimepelekea serikali kwa kiasi fulani kuwa na tahadhari sana na waandishi wa habari.
Wazanzibari watakumbuka kuwa kwa kipindi cha miaka 15 iliyopita kabla ya kuundwa kwa serikali ya Zanzibar yenye mfumo wa Umoja wa Kitaifa, walikuwa wakiishi katika siasa chafu zilizoshadidiwa na vyama viwili vikuu vya siasa. Sitaki niandike sana kuhusiana na miaka hiyo kwani kila siku ninapojaribu kukumbuka ninabubujikwa na machozi ya uchungu. Kwa nini Wazanzibari walifikia mahali walipokuwa wamefikia katika kipindi cha miaka 15? Jawabu ni kwa sababu za kisiasa ambazo undani wake zinalenga kuwanufaisha watu wachache miongoni mwa jamii ya watu wengi. Tusikumbuke huko tukatafuta nani wa kulaumiwa; sote tulihusika.
Moja kati ya makala nilizosoma kuilaumu serikali iliandika kwamba katika kipindi hicho cha siasa chafu, kuna chama ambacho kilipendwa kwa kupendelea vyombo vya habari. Kilivitumia vyombo hivyo kama ni nyenzo muhimu kufikia malengo yake kisiasa wakati serikali ilipokuwa kandamizi. Chama tawala kilikulia kwa kutokuwa karibu na wanahabari kikiwa kimetosheka na nguvu ya dola. Sinahakika juu ya hoja hizi na sina kipimo halisi kiasi gani maadili ya uandishi wa habari yalikuwa yakikiukwa wakati huo na sio ajabu hata leo. Lakini naamini kwamba kwa siasa za wakati huo kila kitu kilikuwa kinawezekana hasa kwa vile ninayajua kwa uhakika makubwa zaidi yaliyofanyika wakati ule kuliko haya; ukiyakumbuka yanatia huzuni.
Nimebaini katika makala nilizobahatika kuzisoma kwamba matarajio ya Waandishi wa Habari hayana tofauti na matarajio ya wananchi wengine wa Zanzibar kwenye serikali yao. Matarajio yao ni makubwa sana kuliko kasi ya mabadiliko inayoendelea katika maeneo mbali mbali.
Makala zote nilizosoma zilikuwa zinaelezea dhana ya kutoshirikishwa waandishi wa habari katika matukio mbali mbali muhimu ya serikali. Matukio zaidi ya mawili yalitajwa kuwa mfano; moja lilikuwa la siku ambayo Dk. Shein aliwaapisha mawaziri wake Ikulu na jengine ni lile la semina elekezi iliyofanyika hivi karibuni kwenye ukumbi wa Zanzibar Beach Resort - Mazizini. Katika tukio la kuapishwa muandishi aliambiwa kuwa waandishi wa habari hawahitajiki katika shughuli hiyo, lakini baadae alikuta waandishi wengi walihudhuria kwenye sherehe hizo na walifanya kazi yao bila ya bugudha. “…..nilifika ikulu mapema na wallahi nilirudishwa nikaambiwa kuwa sherehe ya kuapishwa mawaziri itakuwa ni ya faragha” ……lakini saa mbili baadaye nikawaona waandishi wenzangu kadhaa kadhaa katika viwanja vya ikulu wakishuhudia na kuripoti viapo hivyo” iliandika moja kati ya makala nilizosoma. Hii inajibu kwamba mwandishi ama alipotoshwa au kama alivyosema mwenyewe hakumpata msemaji sahihi na hakumjua yupi msemaji.
Mmoja kati ya waandishi wa makala nilizosoma alielezea hofu yake kwamba huenda waandishi hawakuwa wamealikwa kwenye semina elekezi ambayo alisema ilikuwa muhimu. Sina hakika iwapo mwandishi alikuwa na shida ya nambari ya walioalikwa kwenye semina hiyo au yeye binafsi alitaka aalikwe kwenye semina hiyo. Nasema sina hakika kwa sababu mimi binafsi nilikuwa napata fursa ya kusoma taarifa za mkutano huo kwenye vyombo mbali mbali vya habari na hata kupitia kwenye magazeti hayo hayo yanayolalamika kuwa waandishi hawakushirikishwa. Inanipitikia kuwa dhana ya waandishi sasa imekuwa nyengine.
Nilisoma moja kati maandishi ya makala hizo ikisema “……..kila mwanasiasa alikuwa akiwahitaji kwenye kampeni za kuwania nafasi fulani, jamani fadhila hazipo basi hata hisani haikumbukwi?”. Hili nalo kidogo limenipa hofu na wasi wasi juu ya maadili ya waandishi wetu wa habari. Unapofanya kazi hii kwa nia ya kumfadhili mtu au kwa hisani basi tarajia kulalamika baadae kwa kutoshirikishwa. Uandishi wa habari ni fani, tuiheshimu.
Suala la uhafidhina kwa maana ya watu kutokubali kubadilika pia limezungumzwa sana kwenye makala zote nilizozisoma na kwamba serikali ya Zanzibar chini ya Umoja wa kitaifa inalalia sana kwenye uhafidhina kuliko kukubali mabadiliko na hasa kwa upande wa mawasiliano. Hapa ndipo ninapotafautiana na waandishi wa makala zote na ndipo pale ninaposema labda tulikuwa na matarajio makubwa kuliko uhalisia wa mambo.
Moja kati ya mambo ambayo nimekuwa nikishuhudia ndani ya serikali ya Zanzibar yenye mfumo wa Umoja wa kitaifa ni jinsi ilivyolivalia njuga suala la kuimarisha mawasiliano baina ya serikali na wananchi. Uthibitisho wa hili ni uteuzi wa Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu uliofanywa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na uwepo wa maafisa wa Mawasiliano kwenye Wizara zote za serikali. Hii ni hatua ya ziada, ifahamike pia kuwa serikali inamiliki vyombo kadhaa vya habari kama vile Televisheni Zanzibar, Sauti ya Tanzania Zanzibar, Shirika la Magazeti ya Zanzibar Leo na Idara ya Habari Maelezo.
Lakini jengine linalonithibitishia nia ya serikali katika suala hilo, ni agenda maalum kuhusu mashirikiano kati ya viongozi wa serikali na vyombo vya habari iliyotayarishwa na kuwasilishwa kwenye semina elekezi ya viongozi wakuu wa serikali. Suala hili lilizungumzwa na kujadiliwa kwa urefu sana kwenye semina hiyo na mwisho katika maazimio ilikubaliwa kwamba viongozi wa serikali ni lazima watoe taarifa za shughuli wanazozifanya kwa wananchi.
Kama hiyo haitoshi, katika mkutano wa majumuisho wa ziara yake katika Mkoa wa Mjini Magharibi na Mkoa wa Kaskazini Unguja, Rais wa Zanzibar alisisitiza wito wake wa kuwataka watendaji wa serikali katika ngazi zote kutoa taarifa za serikali kwa wananchi kupitia kwenye vyombo vya habari akisema kuwa wakati wa siasa umekwisha. Waandishi kadhaa walipata fursa ya kuhudhuria kwenye mkutano huu.
Aidha, itakumbukwa kuwa Makamo wa pili wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad kwa bahati mbaya alipofanya ziara yake ya kwanza akiwa kwenye nafasi hiyo katika nchi kadhaa za ughaibuni, hakuwa amechukua waandishi wa habari. Hii ilikuwa ni bahati mbaya na mara tu baada ya kurejea safari hiyo alikiri kuwa alifanya kosa kubwa ambalo hatolirejea tena. Hakuna uungwana kuliko kufanya kosa na kukiri kuwa umefanya kosa. Kubwa zaidi ni kujuta kufanya kosa hilo.
Ninachokisema hapa ni kwamba waandishi tunayo haki ya kukosoa, yapo makosa mengi yanayofanyika na kwa kweli hakuna binadamu asiyefanya kosa. Mwenyezi Mungu tu pekee ndiye mwenye sifa ya kuwa mkamilifu wa kila jambo. Itakuwa inatia mashaka na hatutakuwa tunafanya haki tunapokuwa tunalaumu tu bila ya kupongeza juhudi zinazofanywa na viongozi.
Kuna mengi mazuri yamefanyika chini ya serikali ya Mapinduzi Zanzibar iliyo chini ya Umoja wa kitaifa. Ikumbukwe kuwa miaka 15 ya balaa iliyopita, Wazanzibari ilitukosesha mambo mengi. Kulikuwa na kiwango kikubwa sana cha chuki na uhasama miongoni mwetu mambo ambayo yamesababisha kutokuaminiana. Tulishindwa kukaa pamoja kuzungumzia mambo yetu ya msingi kama Wazanzibari. Wengine walitumia mwanya huo kutunyima haki zetu. Haya yote sasa yameanza kuondoka. Hili peke yake linatosha kuwaletea matumaini makubwa Wananchi wa Zanzibar kwa serikali yao ya Umoja wa kitaifa. Tunapaswa kuwa na mtazamo mpana zaidi wa Zanzibar ya kesho, tufikirie vizazi vyetu vijavyo kuliko ubinafsi.
Lakini moja jengine muhimu zaidi lililozungumzwa kwenye semina elekezi ni kwa Wazanzibari kukubali kubadilika. Kauli hii ilikuwa na maana pana. Tukubali kuwa tunatoka mbali. Kila mmoja anaufahamu wake. Wengine wanafahamu haraka wengine wanachelewa kidogo. Imani zetu pia ni tofauti. Kumbadilisha mtu anachokiamini sio kazi rahisi.
Mmoja kati ya Washiriki wa semina elekezi alikuwa Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Michezo na Utalii. Alisema habari siyo ile ambayo mwandishi anasubiri kupelekewa ofisini au kuitwa akashuhudie mbunge au mwakilishi anagawa mipira ya maji. Waandishi wanatakiwa watafute habari, wafanye uchambuzi, waibue hoja waiambie serikali. Mazuri waseme na mabaya waibue. Uzuri ni kwamba hata uhuru wa vyombo vya habari siku hizi umeongezeka bila ya wenyewe kujua. Kumbe inawezekana vyombo vya habari vya serikali kuandika habari za kuiponda na kuikosoa serikali. Hatuyaoni haya?
Kwa kweli nasema waliokata tamaa na serikali ya Mapinduzi iliyo chini ya Umoja wa kitaifa ni watu wenye matumaini ya mabadiliko ya haraka, hawaoni mbali au watu wenye tamaa binafsi. Vivyo hivyo kwa waandishi ambao wanalia hawashirikishwi kwenye shughuli za serikali. Inawezekana lakini ni vigumu kuwachukua waandishi wote katika shughuli zote. Inatulazimu tukubali kuwakilishwa na wenzetu. Aidha, inawezekana kuweka sawa kila kitu baada ya miaka 15 ya kuhitilafiana lakini ni vigumu. Tusikate tamaa bado ni mapema sana.
No comments:
Post a Comment