Na Luluwa Salum, Pemba
WATOTO 13 waliozaliwa na 19 waliolazwa katika usiku wa kuamkia siku ya mtoto wa Afrika hospitali ya Chake Chake wamezawadiwa zawadi mbali mbali na Wizara ya Ustawi wa Jamii Maendeleo ya Wanawake na Watoto Pemba, ikiwa ni maadhimisho ya siku hio adhimu kwa Mtoto wa Kiafrika.
Akikabidhi zawadi hizo kwa watoto hao Afisa Mdhamini wa Wizara hiyo, Maua Makame Rajab, alisema kwa vile wizara yake ndio inayosimamia haki na wajibu wa watoto imeona ipo haja nao kuungana na wenzao duniani kuadhimisha siku hio kwa kuwatembelea watoto waliolazwa hospitali ili kuwafariji.
Zawadi zilizotolewa hospitalini hapo ni pamoja na nguo za watoto, vinywaji, vifaa mbali mbali vya kuchezea ambavyo vitawasaidia kujifariji kwa muda wote watakapokuwa hospitalini hapo.
Akipokea zawadi hizo kwa niaba ya akinamama waliolazwa na watoto wao hospitalini hapo, Asha Faki Hamad, alisema wamefarijika sana kwa kutembelewa na watendaji wa Wizara ambayo inashughulika na mambo ya wanawake na watoto na wameona ni jinsi gani Wizara hiyo inavyowajali na wanaamini kuwa haitakuwa mwisho kutoa misaada kama hio hasa kwa kina mama na watoto ambao ndio wenye jukumu kubwa la kuwatunza watoto.
Kwa upande wake Katibu wa Hospitali ya Chake Chake, Abushiri Faki Yussuf aliishukuru Wizara ya Ustawi wa Jamii Maendeleo ya Jamii Wanawake na Watoto kwa uamuzi wao wa kufanyia maadhimisho ya mtoto wa Afrika katika Hospitali hio kwa kuwapatia zawadi mbali mbali watoto waliolazwa.
Alisema licha ya kutoa zawadi kwa wagonjwa pia hospitali nayo imekuwa ikikabiliwa na upungufu wa vifaa mbali mbali hivyo ni vyema kulenga katika kusaidia vifaa kama dawa na hata lishe ambayo ni muhimu kwa watoto.
No comments:
Post a Comment