Na Abdulla Mohammed Juma
BAADA ya kuwasilishwa mbele wa Baraza la Wawakilishi, makisio ya mapato na matumizi ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kwa mwaka wa fedha 2011/2012, kilichobakia hivi sasa ni kupewa ridhaa ya wananchi kupitia kwa Wajumbe wa Baraza hilo ambao wanaanza kuijadili kuanzia leo.
Kwa vile bajeti hiyo ni muhimu sana kwa mustakbali wa maisha ya wananchi wa Zanzibar, bila shaka macho na masikio yao yataelekezwa huko ili kuona vipi wanawakilishwa na waliowachagua, itakuwa vyema kwa wawakilishi kuelewa hilo badala ya kujibebesha mzigo wa kudhania kuwa wako 'mjengoni' kwa ajili ya kutoa mawazo yao.
Kuna mambo mengi ambayo yameelezwa katika hotuba hiyo yakiwemo yaliyokuwa wazi na yaliyojificha, pamoja na mazuri na yale ambayo wananchi wangehitaji ufafanuzi zaidi ili kuelewa kilichokusudiwa, kazi ambayo inahitaji kufanywa na Wawakilishi kwa kuitaka serikali kutoa ufafanuzi huo.
SMZ inapaswa kupongezwa kwa kuandaa bajeti ambayo inaakisi mipango ya maendeleo inayoelezwa na Serikali yenyewe, pamoja na kuwapa faraja wananchi kwa kusikia kero kadhaa za muungano zimetatuliwa huku Zanzibar ikianza kufaidika na haki zake kwenye muungano wa Tanzania.
Wajumbe hao hawatoitendea haki serikali wala wananchi wanaowawakilisha, iwapo watasahau kuiboresha bajeti hiyo kwa michang maridhawa inayohusu moja kwa moja maisha ya wananchi na mustakbala wao.
Iwapo hakutotolewa maelezo bayana na Serikali kuhusiana na masuala yaliyoelezwa kwenye bajeti hiyo, wananchi wanaweza baadae kuishutumu serikali kutotekeleza ahadi, kumbe serikali haikuahidi hivyo bali ni kufanya vyenginevyo, jambo ambalo nafasi yake ya kuwekwa sawa ni katika mijadala ya bajeti hiyo.
Haitokuwa busara kwa Wawakilishi kuiga mfano wa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambao wamepoteza muda mwingi wa mjadala wa bajeti wiki iliyopita kule Dodoma kuonesha nao wamo kwa kulumbana na kujijenga kisiasa zaidi ya kuonesha kuwa wanawawakilisha wananchi.
Wawakilishi bado wanao muda wa kuwapitia wananchi wao Majimboni na kuzungumza nao ili waweze kupata maoni na kuyachambua ili wayawasilishe katika michango hiyo ya bajeti kuu ya Serikali, pamoja na bajeti za sekta moja moja zitazokuja baadae katika mkutano huu wa bajeti ya mwaka 2011/2012.
Baraza la Wawakilishi kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo zinapaswa kupongezwa kwa kuandaa semina kutoa darsa maalum kwa Wajumbe hao, ili waelewe mambo mbali mbali yanayohitaji kuchangiwa ili kupusha muda kupotezwa kwa 'blaa blaa' zisizo na faida kwa wananchi, ambazo haziisaidii serikali kuboresha bajeti hiyo.
Mathalan haitokuwa sewe kama Wajumbe hawa wakaitaka Serikali kuainisha kiasilimia namna bajeti hiyo ilivyogawika kwa sekta mbali mbali za huduma za jamii na maendeleo huku ikiainisha tafauti kwa mapana na bajeti iliyopita, lengo likiwa ni kuonesha kweli kama vipaumbele vimejengewa mwega wa utekelezaji ambao unategemea kwa kiasi kikubwa rasilimali fedha.
Huku Zanzibar ikiendelea na kutekeleza mapinduzi ya kilimo, suala la udhibiti wa bei za bidhaa ni lazima lifanyike kwa mamlaka husika kumlinda mtumiaji bila kudaganywa kwamba kutaathiri biashara huria.
Biashara huria haiko Zanzibar peke yake na mfumko wa bei hivi sasa unaeleweka kuenea duniani kote, lakini lazima zitumike njia kama zinazotumika nchi nyengine kudhibiti mfumko wa bei ambao Zanzibar ni wa aina yake kwa kutokwenda hata na mwenendo wa dunia, ambako kuna kupanda na kushuka.
Wawakilishi waelewe kwamba taarifa ya kutopandishwa kodi ya bidhaa iliyoelezwa kwenye bajeti hiyo, wananchi wameipokea vyema, lakini haitokuwa na maana wala tija isipokwenda sambamba na udhibiti wa mfumko wa bei unaofanyika kiholela visiwani Unguja na Pemba.
Upande mwengine haitokuwa vyema kwa serikali kujibinya kutopandisha kodi, huku ikiwaachia wafanyabiashara kujitajirisha kwa kupandisha bei kuongeza ugumu wa maisha kwa wananchi na kuwazidishia umasikini.
Aidha suala linalohitaji kupatiwa ufumbuzi ni namna bei zinavyopanda Zanzibar, mathalan bei ya mafuta ikipanda ulimwenguni ni haki na Zanzibar kupanda, lakini kitendawili kinakuja bi hizo zinaposhuka mbona Zanzibar haziteremki na badala yake huganda pale pale kusubiri zipande tena na kwetu ziongezwe, jambo ambalo ni adimu duniani kote.
Si vibaya Wawakilishi kuitaka serikali kubainisha wazi wazi aina za sekta binafsi, badala ya kuzichukulia kwa ujumla wake, jambo ambalo linaweza kuwaumiza wafanyabiashara wadogo na kuwainua wale wa kiwango cha juu, kwa vile mfumo wa kulipa kodi utakuwa mmoja kwa kodi za kawaida ukiacha ile ya ongezeko la thamani (VAT), ambalo lina viwango vyenye kutambulika wazi.
Inaeleweka kwamba mfumo wa utekelezaji Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini Zanzibar (MKUZA 1) ulikuwa na kasoro na changamoto nyingi, jambo ambalo limetokana na Wizara ya Fedha na Uchumi kubebeshwa mzigo mzito wa kusimamia ambao ulitekelezwa kama kwamba wao ndio watekelezaji, ndio maana ufanisi wake ukawa mdogo.
Katika hili kuna haja ya Wajumbe kuishauri serikali kubadilisha mfumo katika utekelezaji wa MKUZA II, iwe Wizara ya Fedha ni msimamizi wa kweli kweli na si mchezaji na muamuzi, kwani huko ni kuwapa mzigo mkubwa ambao mbali na utaalamu wao hawawezi kufanikisha.
Si sahihi kuona wataalamu wa sekta nyengine kuwa mbumbumbu katika sekta walizobobea, wao ndio wenye kuelewa vipaumbele vya utekelezaji wa mipango ya sekta zao, hvyo wanapowasilisha Wizara ya fedha itekelezwe kama ilivyo na sio kutakiwa kufanya vinginevyo.
Wawakilishi mtambue kuwa wasomi wetu hawa wanaweza kuvunjika moyo na kuiachia Wizara ya Fedha kufanya na kuamua ukiwauliza watasema 'kawaulize Wizara ya Fedha', hapo maendeleo kwa wananchi yatakuwa ndoto na ufanisi ya MKUZA II utakuwa wa maneno kama ilivyokuwa ule MKUZA I.
Kwa vile Wawakilishi mnaelewa kwamba MKUZA II ndiyo Dira ya maendeleo ya Zanzibar kuanzia bajeti hii ya mwaka 2011/2012 ni vyema mkaishauri Serikali kuwa utekelezaji wake uzingatie tathmini ya MKUZA I kwa kufuata ushauri utaotolewa, lakini uwe umefanyika kihalisia badala ya kuchukua yale yale mawazo ya Wizara ya Fedha ambayo imejifanyia tathmini yenyewe, ambapo ingekuwa kesi waswahili wangesema sawa na kumshitaki kima kwa tumbili, hukumu yake ndiyo itakuwa jibu la tathmini hiyo.
Wawakilishi mna dhima ya kuhakikisha bajeti hii inapanga mipango kabambe itayotekelezeka ya kuwawezesha wananchi kuuelewa MKUZA moja kwa moja, kwani changamoto kubwa ya mpango huo awamu ya kwanza ni elimu ndogo iliyotolewa kwa wananchi kiasi kudhani kuwa MKUZA ni kupewa fedha mfukoni za kununua mchele na samaki kula na watoto nyumbani.
Hilo lilisababishwa zaidi na kutoshirikishwa ipasavyo kwa vyombo vya habari vikiwemo vile vya umma kama gazeti la Zanzibar Leo, Televisheni Zanzibar (TVZ) na Sauti ya Tanzania Zanzibar (STZ), ambazo zilikuwa zikitumika pale tu panapohitajika kutolewa ufafanuzi baada ya vyombo visivyo vya serikali kutoa taarifa dhidi ya utendaji wa taasisi au mtendaji fulani wa Serikali.
Kuna haja katika utekelezaji wa mipango ya serikali ikiwemo MKUZA II kwenye bajeti hii kuwepo utaratibu wa kuvitumia vyema vyombo hivi si tu kupanua utekelezaji wa emokrasia na utawala bora, bali pia kuwaelimisha wananchi haki na wajibu wao katika utekelezaji miradi hiyo 77 na programu 27 zilizomo ndani ya bajeti hiyo.
Hilo litawezekana iwapo Wawakilishi watahakikisha serikali inaviwezesha vyombo hivyo kihali na mali, kwan hivi sasa STZ bado inahema, lakini TVZ imedhoofika kiasi cha kuwakosesha taarifa muhimu wananchi wa Pemba kwa aidi ya mwaka mmoja sasa na gazeti pekee linalotengenezwa Zanzibar la 'Zanzibar Leo' kuendelea kutumia mamilioni ya fedha za mapato yake kwa kuchapisha magazeti yake ya kila siku katika viwanda vya Tanzania Bara, kutokana na ukweli kwama hadi leo hii Zanzibar kunakosekana mitambo ya kuchapishia magazeti ya rangi.
Watendaji na wafanyakazi wa vyombo hivyo bado wanachukuliwa kama wafanyakazi wengine wa Serikali, japokuwa inaeleweka kwamba mazingira ya kazi zao ni magumu na maalum, hivyo ni lazima waangaliwe kimaslahi ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo, vyenginevyo tutaendelea kuwalaumu na wananchi hawatofaidika na vyombo hivyo, huku kila anaeng'ara kuvikimbia kufuata maslahi bora kwengine.
Uundwaji wa Mashirika ya umma ni suala jengine ambalo Wawakilishi wanapaswa kuisaidia serikali kuachana na mfumo wa sasa wa kubadilisha taasisi majina kuwa mashirika bila ya kuzpa nyenzo kama vile mitaji ya kuanza kujiendesha kishirika, jambo ambalo linayafanya kuwa mzigo kwa serikali, kwani badala ya kuisaidia Serikali zinabakia kuwa tegemezi kwa kusubiri ruzuku kutoka serikalini.
Mengi cha ajabu hata miundo yake hubakia kama ilivyo na kung'ang'ania rundo la wafanyakazi wasiozalisha.
Taarifa njema ya kupanda kwa pato la mwananchi ni lazima liainishwe vipi litafikiwa, kwani habari hiyo inaweza kuwa ndiyo sababu ya watendaji wa serikali kubweteka na wananchi kusubiri kupewa fedha mfukoni badala ya kuwajibika, ni lazima kipengele hicho kifafanuliwe zaidi kwa wananchi kuarifiwa majukumu ya kufikia huko.
Matarajio ya wananchi kwa Serikali yao ya Mapinduzi ya Zanzibar, ambayo iko katika mfumo mpya wa umoja wa kitaifa yanategemea zaidi bajeti hii kwa kuazia, hivyo michango ya Wawakilishi haitegemewi kutawaliwa na malumbano ya kisiasa kama ilivyokuwa huko nyuma, bali mafanikio ya serikali ya mfumo huo mpya ambao vyama vyenu ndivyo vilivyoiunda.
0777 471199
abdulladulla@hotmail.com
No comments:
Post a Comment