Na Halima Abdalla
KATIBU Mkuu Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Zanzibar (ZATUC) Khamis Mwinyi Mohammed, amesema endapo shirikisho hilo halitaridhishwa na kima cha chini ya mshahara ambacho hivi sasa kimekuwa siri, hakitakubaliana na bajeti ya serikali.
Katibu huyo alieleza hayo jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari huko ofisini kwake Kikwajuni mjini hapa ambapo Wizara ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ni lazima ijitahidi kukidhi majitaji ya wafanyakazi.
''Suala la maslahi ya wafanyakazi halikuelezwa bayana na tumeambiwa waziri mwenye wizara inayohusiana na Utumishi wa Umma ndie atakaelezea,
hivyo kama hatukuridhishwa na majibu yake hatutaiunga mkono bajeti hiyo katika kipengele cha mishahara ya wafanyakazi,''alisema Mwinyi.
Aidha aliipongeza serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kupunguza kiwango cha kodi kwa wananchi katika bajeti hiyo na kuwaomba kufanya uwezekano wa kupunguza zaidi ili kuwapunguzia wananchi makali ya maisha.
Akiichambua bajeti hiyo alisema serikali ilitakiwa itambuwe sekta isiyo rasmi katika bajeti kuliko kutegemea kutoka nje kwani suala hili linaifanya bajeti kuwa tegemezi.
Aidha aliishauri serikali katika bajeti hiyo wanapoboresha majengo ya wafanyakazi kuangalia ujenzi ambao utaruhusu na watu wenye ulemavu kufika kueleza mahitaji yao.
Sambamba na hayo aliishauri serikali ipokee maoni ya wadau mbali mbali ikiwemo vyama vya wafanyakazi katika kuboresha zaidi bajeti hiyo.
Aidha alisema bajeti ni kubwa aliishauri serikali kujipanga zaidi katika kuhakikishwa bajeti hiyo inatekelezwa.
No comments:
Post a Comment