Amesema hatua hiyo ni muhimu katika uhifadhi wa mazingira pamoja na kuirejesha ardhi uhai wake ili iweze kutumika kwa miaka mingi ijayo.
Maalim Seif amesema hayo huko Vitongoji Uwandani, alipozungumza na wachimbaji wa matofali, katika ziara yake ya kufuatilia utekelezaji wa agizo la Serikali la kufukia mashimo yote yaliotokana na shughuli za uchimbaji na upasuaji wa matofali, katika eneo linalokadiriwa kufikia ekari 28.
Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilio katika mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, haina nia ya kuwaonea au kuwanyanayasa wananchi wake pamoja kuwaona wanaishi maisha ya taabu.
Alisema pale wananchi wanapoitikia maagizo ya Serikali, kamwe hapawezi kutokea ugomvi, au Serikali kulazimika kutumia nguvu za ziada kukabiliana na hali iliopo.
Alibainisha kuwa hatua inayoendelea hivi sasa ni muhimu kutekelezwa ili kufikia azma ya serikali ya kuhifadhi mazingira pamoja na kuhakikisha ardhi ndogo iliopo inakifaidisha kizazi kijacho.
Aliwakumbusha wachimbaji hao umuhimu wa utekelezaji wa mikataba iliowekwa kati yao na Serikali na kusisitiza haja ya kuchimba mashimo yasiiozidi mita tatu.
Aidha alitanabahisha kuwa Serikali italazimika kuchukuwa hatua kali za kisheria dhidi ya wakorofi wachache wanaokaidi agizo la Serikali au kwenda kinyume na mikataba waliofikia.
Maalim Seif alisema ni lengo la Serikali kupitia Wizara ya Kazi,Ajira na Uwezeshaji wananchi Kiuchumi, kuwapatia kazi mbadala wachimbaji hao ili waweze kujikimu kimaisha pamoja na kuondokana na hatari ya kupata maradhi mbali mbali kutokana na vumbi wanalomeza kila siku.
Aliwataka wachimbaji hao kujikusanya na kuanzisha vikundi vya pamoja, huku Serikali ikiwa mbioni kuwatafutia miradi mbadala wanayotaka kuifanya ili waweze kuendesha maisha yao .
Aidha alitoa wito kwa Wizara ya Uvuvi kukaa pamoja na wananchi hao, kuangalia mahitaji waliyonayo ili waweze kuitumia sekta hiyo.
Mapema Naibu Katibu Mkuu,Ofisi ya Makamu wa kwanza wa Rais, Dk.Islam Seif alisema utaratibu unaotumika hivi sasa wa kufukia mashimo hayo ni mfumo tu wa kurejesha mazingira ya ardhi, lakini ni vigumu mno kurejesha uhalisia wake kwa miaka mingi ijayo.
Alisema kazi hiyo inahitaji mashirikiano makubwa kati ya Serikali na wananchi, ambapo hadi sasa ni ekari tano tu zilizofanikiwa kufukiwa kutoka ekari 28 zilizoharibiwa kabisa.
Alizishauri idara zinazohusika, ikiwemo ya Misitu,Ardhi na Mazingira kukaa pamoja na kufanya upembuzi wa maeneo yanayofaa kutumiwa kwa shughuli hizo badala ya kuendelea na utaratibu uliopo, kwa wachimbaji hao kuchimba popote pale hata katika maeneo yanayofaa kwa kilimo.
Nae Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Juma Kassim Tindwa, alieonekana kuwa na mawazo tofauti, uliainisha ugumu uliopo katika kulipatia ufumbuzi suala hilo, akiwatuhumu wananchi wa maeneo hayo kuwa wengi wao ni wakarofi.
Akinasibisha na kauli yake, Tindwa alisema mbali na wachimbaji hao kupewa taarifa ya ujio wa Makamu wa Kwanza wa Rais na kutakiwa kufika kumsikiliza, lakini wao walioendelea na shughuli zao za uchimbaji kinyume kabisa na mikataba yao inavyowataka.
Alisema mbali na wachimbaji hao kupewa fomu ili waanzishe vikundi kwa ajili ya miradi mbadala, wameshindwa kabisa kurejesha fomu hizo, tofauti na wachimbaji wenzao wa kwa Sanani Muwambe ambao tayari wameunda vikundi 18.
Alisema kuna dhana iliojengeka katika nyoyo za watu hao kuwa kazi hiyo ya kudumu na ndio sababu mbali na kupewa fomu hizo wameshindwa kuzirejesha.
Alimtaka Mkuu wa Wilaya hiyo kwa kushirikiana na kiongozi wa wachimbaji, Ali Kombo ‘Mbunge”, kuwaondoa wafedhuli wote katika machimbo hayo kama njia ya kufikia lengo la Serikali , na iwapo itashindikana uongozi wa Mkoa wake uliahidi kuchukua hatua dhidi yao.
No comments:
Post a Comment