Na Hassan Hamad
MAKAMU wa kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amewataka waislamu nchini kuyatumia mafunzo waliyoyapata katika mwezi mtukufu wa Ramadhani kwa kuendeleza umoja na mshikamano ili kuiendeleza dini ya Kiislamu.
Amesema iwapo waislamu wataungana na kushirikiana wanaweza kuleta mabadiliko ya kimaendeleo na kukuza thamani ya dini yao ndani na nje ya nchi.
Maalim Seif ameeleza hayo jana katika ukumbi wa hoteli ya STAR LIGHT, jijini Dar es Salaam wakati akitoa shukrani kwa waislamu walioitikia wito na kujumika pamoja katika futari aliyoandaa na kuwashirikisha watu mbali mbali wakiwemo Masheikh, Maimamu na waumini kutoka Mkoa wa Dar es Salaam.
Alisema waislamu wna wajibu mkubwa wa kumcha Mwenyezi Mungu katika umri wote wa maisha yao na kuwataka kuondokana na dhana kuwa suala la ibada ni kwa ajili ya mwezi mtukufu wa Ramadhani pekee.
Aliwataka kuishukuru neema ya Mwezi mtukufu wa Ramadhani kwa kuendeleza mafunzo waliyoyapata, kwa kigezo kuwa mwezi wa ramadhani ni darasa tosha kwao kujifunza mambo mazuri, ikiwa ni pamoja na kuthaminiana na kuhurumiana katika maisha ya kila siku.
Aidha aliwataka waislamu kuzingatia umuhimu mkubwa wa kushikamana na kuondoa atofauti miongoni mwao ili kujenga nguvu itakayowawezesha kupigania haki zao.
Alisema waislamu wana mahitaji mbali mbali ambapo itakuwa ni vigumu kuweza kupatikana iwapo hakutakuwepo na umoja na mshikamano
Mapema akitoa shukrani kwa niaba ya waalikwa wa futari hiyo , Sheikh Mussa Kundecha kutoka Dar es Salaam amewasisitiza waislamu kuendeleza tabia njema na kuondosha tofauti zao, na kwamba kufanya hivyo kutaupa nguvu zaidi uislamu.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na Viongozi na waislamu wa madhehebu mbali mbali nchini, pamoja na Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi CUF Taifa Profesa Ibrahim Lipumba.
No comments:
Post a Comment