Habari za Punde

DK SHEIN ATEUA KAMISHENI YA UTUMISHI WA UMMA

Amuanika Vice Chancellor mpya wa SUZA
Atandika uongozi Bodi ya mikopo elimu ya juu
Ateua Wenyeviti Bodi nne za umma
Atangaza Makadhi sita wa wilaya

Na Mwandishi wetu

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk.Ali Mohamed Shein, amefanya uteuzi wa viongozi mbali mbali za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar jana.


Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Dk.Abdulhamid Yahya Mzee, Dk.Shein amemteua Mohammed Fakih Mohammed kuwa Mwenyekiti wa Kamisheni ya Utumishi wa Umma Zanzibar kwa mujibu wa sheria ya Utumishi wa umma nambari 2 ya mwaka 2011.

Katika kukamilisha Kamisheni hiyo, Dk.Shein pia amewateua Wajumbe wa Kamisheni hiyo ambao ni Hamid Mahmoud Hamid, Mabrouk Jabu Makame, Issa Mohammed Suleiman, Ali Rajab Juma, Balozi Hussein Said Khatib na Jecha Salim Jecha.

Pia taarifa hiyo imeeleza kuwa Dk.Shein amemteua Profesa Idris Ahmada Rai kuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kwa kutumia kifungu cha 9 (1) cha sheria ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar nambari 8 ya mwaka 1999.

Aidha Dk.Shein kwa kutumia kifungu cha 4 (1) (a) cha sheria ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu nambari 3 ya mwaka 2011, amemteua Kombo Hassan Juma kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu Zanzibar na kumtangaza Iddi Khamis Haji kuwa Mkurugenzi wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu Zanzibar.

Katika hatua nyengine, Dk.Shein ameteua wenyeviti wa Bodi katika taasisi mbali mbali za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Wenyeviti walioteuliwa na Bodi zao kwenye mabano ni Salmin Senga Salmin (Shirika la Bandari Zanzibar), Mwalim Haji Ameir (Shirika la Meli na Uwakala Zanzibar), Dk. Issa H. Ziddy (Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana Zanzibar) na Mariam Mohammed Hamdan (Hakimiliki).

Kwa kutumia kifungu cha 5 cha Sheria ya Mahkama ya Kadhi nambari 3 ya mwaka 1985 kama ilivyorekebishwa na Sheria nambari 4 ya mwaka 2003 kifungu cha 5, Dk.Shein amewateua Makadhi wa wilaya sita.

Walioteuliwa ni Sheikh Mustafa Hassan Mwinyi, Sheikh Ali Khamis Mussa (Kidemere), Sheikh Mansab Khamis Omar, Sheikh Mohammed Ali Hamad, Sheikh Nassor Khamis Mbawana na Sheikh Daud Khamis Salim.

Taarifa hiyo ya Dk. Abdulhamid imeeleza kuwa uteuzi huo unaanza leo tarehe sita Septemba 2011.

6 comments:

  1. Mbona hatukupata picha za shamrashamra za VC mpya wa SUZA au harusi bado ilikuwa Akdi ya siri tu?

    ReplyDelete
  2. Sijui Dk.Ziddy atasaidiaje kuokoa zile nyumba za wakfu ambazo zinakodishwa karibu na bure na hivyo kamisheni ya wakfu kushindwa kuzifanyia matengenezo stahiki na hatimae kuanguka na kukatiza "swadakatul-jariyya" za marehemu na kwenda kuwa mass-ul? Tukumbuke jamani hawa watu walitoa muhanga mkubwa kuweka nyumba zao wakfu! hivi mnajua kua siku hizi hamna kitu cha namna hiyo,kutokana na watu kupenda sana mali na dunia?

    ReplyDelete
  3. Very simple,ni kutumia bei ya soko tuu.Ila mimi kero yangu ni tofauti,ni kuhusu vile vyeti vya ndoa,hivyo wadau ni lazima vyeti vile viandikwe na watu wasiokwenda skuli, au wanaojua kiarabu kiswahili? hivi serekali ina jua kua vile vitabu mashehe wanavitoa copy na kufanya watu 2 walio na vyeti kutumia reference no.1? jamani tuwe makini vyeti sku hizi vinafika mbali tofauti na zamani..commissioner ziddy atusaidie katika hili pia...MUNGU ISAIDIE ZANZIBAR.

    ReplyDelete
  4. Dr. Shein amefanya vyema kutomteuwa tena Ali Mzee Ali kuwa mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la meli na Uwakala, Mzee alikuwa "corrupt" na mharibifu wa makusudi na amechangia sana kurudisha nyuma juhudi za shirika kupata meli mpya. Kadhalika ndiye aliyepanga project ya kifisadi ya ununuzi wa meli mpya kwa kiasi cha dola za kimarekani milioni 25, ambazo ni nyingi kupita thamani halisi ya chombo hicho na upya wake, thanks Dr. Shein alishituka na kukataa mpango ule wa kifisadi wa Ali Mzee na watu wake, ombi kwa Mhe. Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano, Mhe. Hamad Masoud Hamad, ambaye anadhamana ya kuteuwa wajumbe walibaki wa bodi ya shirika la meli, ahakikishe hamrejeshi mjumbe yoyote wa iliyokuwa bodi ya Ali Mzee kwa kuwa wote walikuwa mafisadi.

    ReplyDelete
  5. Ahsanteni kwa comments, naamini wahusika watakuwa wanapitia na kuziona.

    Picha za shamrashamra hatuna ila nadhani ni hatua muhimu kuwarudisha nyumbani Vijana kama kina Profesa Rai kuja kushikamana katika kuliendeleza Taifa letu.

    Mlio katika Diaspora ughaibuni kina Rai wameshaonesha mfano...

    ReplyDelete
  6. Kaka naamini wadau watarudi,ila bado wanaskilizia.Unajua tena mambo yetu, unaweza ukaona "juu kukavu kumbe chini bado"

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.