Habari za Punde

MIRADI YA CHINA ITAWANUFAISHA WAZANZIBARI - BALOZI QIMAN


Na Ramadhan Makame

BALOZI Mdogo wa China nchini Tanzania aliyepo Zanzibar, Chen Qiman amesema nchi yake itaendelea kuisaidia Zanzibar kwenye miradi mbali mbali yenye lengo la kuwaletea maendeleo na kuinua hali za maisha ya wananchi.

Balozi Chen alieleza hayo hoteli ya Zanzibar Beach Resort iliyopo Mazizini, wakati alipokuwa akitoa hotuba ya kuadhimisha siku ya taifa la China kufikia miaka 62 hapo juzi.


China imekuwa ikisaidia na inataka kusaidia miradi kama vile ya miundombinu, teknolojia ya habari na mawasiliano, afya, elimu, maji pamoja na kusaidia elimu kwa rasilimali watu.

Alisema miradi ambayo China imekuwa ikiisaidia Zanzibar inalenga kuinua hali za maisha ya wananchi kiuchumi na kijamii na kuahidi kuwa miradi hiyo itakamilika katika kipindi cha miaka miwili ya utumishi wake visiwani hapa.

“Ningependa niwaeleze kuwa miradi hii itakamilika katika kipindi changu cha miaka miwili ambayo nitakuwa hapa, na hilo litanifurahisha na kunipa faraja sana”,alisema Balozi Chen.

Aidha alisema ipo siku wananchi wa mji wa Zanzibar, wataushuhudia mji wao uking’ara kwa taa barabarani, kwani wataalamu wa nchi hiyo wataweka taa hizo ambazo zitakuwa zikitumia umeme wa nguvu za jua.

“Tuna miradi ya ujenzi wa wodi ya wagonjwa mahatuti (ICU), katika hospitali ya Mnazimmoja na ujenzi wa skuli za sekondari, miradi hii tunaahidi tutaikamilisha katika kipindi kifupi kijacho”,alisema Balozi huyo.

Akizungumzia kuhusu kusaidia rasilimali watu, alisema katika kipindi cha mwaka mmoja maofisa zaidi ya 200 wa ngazi ya juu kutoka serikali ya Zanzibar watapata nafasi ya kujifunza mambo mbali ya juu ya maendeleo ya China, ambayo kama watayatumia Zanzibar nayo itapiga hatua kubwa za kimaendeleo.

Alisema maendeleo ya kiuchumi yaliyofikiwa na China, faida yake itawanufaisha marafiki katika nchi mbali mbali za Kiafrika ikiwemo Zanzibar, ambayo imekuwa ikfaidia na maendeleo hayo.

Kwa upande wake mgeni rasmi katika hafla hiyo, waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Haji Omar Kheir, alisema Zanzibar inajivunia uhusiano wake na China na urafiki huo umekuwepo kwa muda mrefu.

Waziri Kheir alifahamisha kuwa China ilikuwa na nchi ya kwanza kuitambua Zanzibar baada ya Mapinduzi ya mwaka 1964, na kwamba uhusiano uliopo hivi sasa unatokana na misingi imara iliyowekwa na waasisi wa mataifa hayo.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbali mbali wa serikali, mabalozi pamoja na raia wa China waliopo Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.