Habari za Punde

TUME YA MV SPICE KIINI MACHO

Salim Said Salim

SASA ni wiki mbili toka kuundwa tume ya watu 10 kuchunguza kuzama kwa meli ya Spice Islander iliyosababisha vifo vy watu zaidi ya 240 na abiria zaidi ya 500 kutoonekana na kusadikiwa wamekufa na zaidi ya watu 600 wameokolewa.

Mengi yamesemwa kuonesha mashaka juu ya muundo wa tume hiyo, lakini malalamiko hayo hayakupatiwa ufafanuzi na hii imetoa tafsiri kwamba viongozi wa serikali na walioelezwa kuwa hawakustahiki kuwa katika tume hiyo, hawana utetezi.


Hali hii haishangazi kwa sababu bado katika nchi yetu tunaendeleza utamaduni wa kudharau maoni ya wananchi kama vile hawana haki ya kukosoa na kushauri. Wanachotarajiwa ni kukubali kila wanaloambiwa.

Hata hivyo, baadhi yetu tutaendelea kutoa maoni na ushauri, japokuwa tunajuwa tunalofanya ni sawa na kuzungumza na ukuta.

Historia itatuhukumu kwa mchango wetu na pia kuwahukumu wanaodhani na kuamini wao tu ndio wenye maamuzi na wengine ni sawa na abiria waliopo kwenye basi na hawajuwi wanapelekwa wapi na hawana haki ya kuuliza.

Tume imeshaundwa na kwa bahati mbaya hatujaelezwa hadidu rejea zake na haikupewa muda wa kufanya kazi na kutoa ripoti. Hii ina maana inaweza kuchukua miezi mitatu au mitano kwa sababu inategemea wajumbe wake watakavyopenda.

Kama hii tume inataka wananchi waamini imefanya kazi inayotarajiwa yafuatayo ni miongoni mwa mambo ambayo watu wanataka kupatiwa maelezo ya kina.

Ni miaka mingapi toka hii meli kuundwa. Ni muhimu kwa sababu inasemekana ni miaka 44 na baadhi ya wataalamu wanasema kwa kawaida muda wa matumizi ya meli katika bahari ni miaka 40. Ukweli ni upi?

Lini mara ya mwisho meli hiyo ilikaguliwa ili kuthibitisha kuwa ni salama kwa usafiri wa abiria?

Kwa kawaida ukaguzi unatakiwa ufanywe baada ya muda gani na ukaguzi wa mwisho ulifanywa na mtu mmoja au zaidi na kama haukufanyika kwa nini na nani alitarajiwa kuufanya?

Nani mwenye mamlaka ya kuruhusu meli kufanya safari na kabla ya kutoa ruhusa anapaswa kufanya nini na je, hili lilifanyika kabla ya Spice kuondoka bandarini kulekea Pemba?

Meli ya Spice imesajiliwa kuchukuwa abiria wa ngapi na kiasi gani cha mzigo. Je, ilipoondoka ilikuwa na abiria wangapi na mabaharia wangapi? Palikuwapo orodha ya abiria (manifesto)? Nani aliitenengeneza na aliridhika idadi ya abiria alioyoorodhesha ilingane na ile ya watu waliokuwamo ndani ya meli?

Meli ya Spice ilikuwa na makoti ya uokozi mangapi na lini mara ya mwisho kukaguliwa na kuonekana yote mazima na yanaweza kumuokoa mtu wakati wa hatari?

Hii meli ilikuwa na mabaharia wangapi na kati yao wangapi wanajuwa kuogelea na kuokoa watu wasizame? Lini mara ya mwisho wamefanya mazoezi ya uokozi?

Hapo bandarini panakuwepo kundi kubwa la askari polisi, KMKM na maofisa wa uslama wa taifa. Watu wanataka kujuwa nini hasa kinawapeleka hapo na kama ni usalama wa abiria walikuwa wapi meli ilipokuwa ikiondoka?

Zipo habari kutoka vyanzo vingi vya habari ikiwa ni pamoja na watu waliokoka na abiria waliokuwa wakiwasiliana na jamaa zao wakati meli ilipokuwa inazama, kwamba baadhi ya watu walipoona meli imesheheni vibaya walitaka kuteremka, lakini walizuwiwa.

Ukweli wa jambo hilo unatafutwa na kama ni kweli ni nani hao waliowazuia watu na kwa sababu gani walifanya hivyo?

Kikosi cha uokozi kiliagizwa kutoka Afrika Kusini lakini kilichojitokeza ni kwa watu hawa kuja kama watalii. Walishindwa hata kukaribia nusu ya kina cha maji cha mkondo wa Nungwi.

Nani hasa aliwaita na je, walielezwa kwamba meli imezama katika kina cha maji ni cha zaidi yamita 300? Kiasi gani cha fedha kilitumika kwa zoezi hili liliokuwa halina mafanikio.

Tume hii inapaswa ielewe kwamba watu wa Zanzibar na Tanzania kwa jumla wamechoshwa na uzembe, jeuri, kibri na dharau zinazoonekana kufanywa kwa watu wanaotumia usafiri wa baharini.

Tumeshuhudia meli zikigongana baharini na watu kufa, meli kuishiwa mafuta katikati ya safari, kufanya safari bila ya maji kwa matumizi ya abiria, kutofuata ratiba, misongamano ya abiria na kufanya safari bila ya daktari wala muuguzi.

Baadhi ya mambo ni uhuni uliovuka mipaka. Mfano ni wa nahodha (kama alivyofanya wa mv Mapinduzi), kukataa amri ya kumzuia kusafiri kwa sababu meli ilikuwa imejaza sana na kuegemea upande mmoja na badala yake kwa kiburi na jeuri ikafanya safari ya Mtwara,

Meli pia hukawia kuondoka bandarini kwa kungojea wanafamilia wa mmiliki wa chombo wakiwa wanamaliza kunywa chai nyumbani.

Haya na mengine mengi ya kusikitisha na kutisha ndiyo majaliwa wanayokutana nayo wasafiri wa vyombo vya baharini. Tume inatakiwa iyaangalie yote haya na kutoa mapendekezo yatakayoweka utaratibu mzima na kuheshimu maisha na utu wa wasafiri.

Mfululizo wa maafa yaliyotokea katika siku za hivi karibuni yanatosha na njia pekee ya angalau kuwapunguzia vilio vya kila siku ni kuchukuliwa hatua thabiti za kuwa na usafiri wa usalama na kila anayezembea awajibishwe kisheria.

CHANZO: Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.