Habari za Punde

VIONGOZI WA DINI WATOA POLE KWA RAIS

Na Rajab Mkasaba

VIONGOZI wa dini kutoka Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Ofisi za Mufti na Kadhi Mkuu Zanzibar pamoja na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), wametoa mkono wa pole kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein kufuatia kuzama kwa meli ya MV Spice Islander hivi karibuni.


Uongozi huo ulieleza hayo wakati ulipofika Ikulu mjni Zanzibar kwa lengo la kumpa mkono wa pole Rais Dk. Shein, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na wananchi wote wa Tanzania hasa wa Zanzibar kufuatia msiba huo uliolikumba Taifa.

Viongozi hao wa dini wa Kitaifa, ulieleza kuwa wamepokea msiba huo kwa masikitiko makubwa na kutoa shukurani kwa Mwenyezi Mungu kwa mapenzi yake aliyonayo kwa binaadamu hasa kuwezesha watu zaidi ya mia tano kusalimika katika ajali hiyo.

Walieleza kuwa mara baada ya kupokea taarifa hiyo wao viongozi wa dini wamekuwa wakisali na kuomba dua kwa ajili ya waathirika wote wa ajili hiyo waliofariki, waliojeruhiwa, familia za wafiwa na waliojeruhiwa pamoja na serikali.

Aidha, viongozi hao wa dini walitoa pongezi zao kwa Dk. Shein, serikali anayoiongoza pamoja na wananchi kwa juhudi zilizofanyika katika kuokoa watu kadhaa na kumuombea Dk. Shein kwa MwenyeziMungu kuwa na nguvu ya kuendelea kuwatumikia wananchi.

Pamoja na hayo, viongozi hao walitoa pongezi zao kwa Dk. Shein kwa uwamuzi wa kufanya uchunguzi wa ajali hiyo na kueleza kuwa wanamatumaini makubwa kuwa uchunguzi huo utafanywa kwa makini na uwazi ili kubaini chanzo cha ajali hiyo.

Viongozi hao wa dini pia, walitoa rambirambi zao kwa kukabidhi fedha taslim milioni 2 kama alama na ishara ya mshikamano wao katika msiba huo.

Viongozi hao wa dini waliofika Ikulu ni Askofu Mkuu Valentino Mokiwa, Askofu Mkuu Alex Malasusa, Sheikh Mohamed Muhenga, Sheikh Mokhamed Khamis Said, Askofu Agostino Shao, Padre Anthony Makunde, Padre Damas Mfoi, Sheikh Nouman Jongo, Sheikh Talib Abdalla, Pete Maduki na Sheikh Fadhil Soraga.

Nae Dk. Shein alitoa shukurani kwa ujio wa viongozi hao na kueleza kuwa uwamuzi wao huo ni mzuri na wa busara.

Alieleza kuwa Zanzibar ina historia kubwa katika usafiri wa bahari kwa miaka mingi lakini wananchi wake na mabaharia wanaofanya kazi kwenye vyombo hivyo hawajawahi kupata msuko suko kama huo.

Dk. Shein alieleza kuwa ujio huo wa viongiozi wa Dini kutoka Zanzibar na Tanzania Bara umempa faraja kubwa na kumpa nguvu katika kutekeleza kazi zake za kuwatumikia wananchi kwa mashirikiano ya pamoja.

Katika maelezo yake Dk. Shein alisisitiza kuwa ahadi yake ya kuunda Tume ya uchunguzi ni ahadi aliyoitoa ndani ya nafsi yake kwa lengo la kujua sababu na chanzo cha ajali hiyo ili kuepukana na kutokea janga jengine kama hilo.

Aliwahakikishia viongozi hao kuwa Tume hiyo itakuwa na watu waliobobea katika fani ya vyombo vya baharini.

Aidha, Dk. Shein aliueleza ujumbe huo kuwa juhudi za uokozi bado zinaendelea licha ya changamoto zilizojitokeza.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.