Habari za Punde

TAASISI ZA AL MADINAH NA KLABU YA SAIGON YATUMA SALAMU ZA RAMBIRAMBI

Salama Juma, Maelezo

TAASISI ya Al-Madinah Social Service Trust na Klabu ya Saigon zimetuma salamau za rambirambi kwa wazanzibari na watu wote waliopoteza ndugu zao kufuatia kuzama kawa Meli ya MV.Spice Islander katika Pwani ya kijiji cha Nungwi wilaya ya kaskazini Unguja mnamo tarehe 10 septemba , mwaka huu.


Akitoa salamu hizo jijini Dar es salaam, Mwenyekiti wa Taasisi ya Al-Madinah - Social Service Trust Sheikh Ally Mubarak, amesema kuwa wamepokea kwa masikitiko na huzuni kuzama kwa Meli hiyo na ambayo imepoteza maisha ya watu zaidi ya 200 na kunusuru takribani watu 600 ambao pia wameumizwa kisaikolojia.

Sheikh Mubarak anamuomba Mwenyezi Mungu awapumzishe salama wote waliofariki kwenye ajali hiyo na awape nguvu majeruhi na wafiwa wote, amewaomba wafiwa kuwa na subira katika kipindi hiki kigumu kwa kuondokewa na wapendwa wao pasipo mategemeo.

Sheikh Mubarak amesema kuwa utawala wa sheria na uongozi bora ndio suluhisho la majanga haya na kwamba wakati umefika wahusika wawajibike au wawajibishwe kwa uzembe wa kutofuata taratibu na sheria za kazi za taaluma husika.


Aidha Sheikh Mubarak amewakumbusha wote wanaopewa dhamana ya kuhudumia abiria katika barabara , maji , anga na reli kuwa makini na kufuata sheria za taaluma zao ili kuepuka kuliingiza taifa katika majanga kama la MV Spice Islander.

“Wakati tukiomboleza Taasisi ya Al-Madinah Social Service Trust na Klabu ya Saigon zinawakumbusha wote wanaobeba dhima ya kuhudumia wenzao katika Nyanja zote ikiwemo barabara,maji , anga na reli kuwa makini na kufuata sheria za taaluma zao ili kuepuka kuliingiza taifa katika majanga kama hili la MV Spice Islander”.Alisema Sheikh Mubarak.

Sheikh Mubarak amepongeza serikali na viongozi wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa juhudi za makusudi na zilizotukuka walizozionyesha wakati wote wa tukio hilo la kuzama kwa Meli hiyo.

Amesema kuwa taasisi hiyo inaungana na Taasisi nyingine zote za kiserikali, kijamii, kidini , kielimu na kiuchumi katika kuomboleza msiba huu mkubwa wa kitaifa uliomgusa kila mmoja wetu hapa nchini ukikumbusha msiba mkubwa wa MV bukoba uliotokea mwaka 1996 iliyosababisha vifo zaidi ya watu 800 na kujeruhi wengine kadhaa na kupoteza mali za watu

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.