Habari za Punde

WIZI WA KARAFUU NI JAMBO LA KAWAIDA TU, BALOZI SEIF AAMBIWA


Tabia ya wizi wa karafuu unaoendelea kufanywa na baadhi ya watu katika mashamba ya Serikali unapelekea kupunguza mapato ya Wanaokodi zao hilo Kisiwani Pemba.

Bwana Khamis Salum maarufu Cholo ambae mara kadhaa hukodi mashamba ya karafuu ya Wilaya ya Wete ameiambia Kamati Maalum ya Serikali inayoshughulikia Mashamba ya Serikali ikiongozwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kwamba watu hao mara nyingi huendesha wizi huo wakati wa usiku.


Bwana Khamis Cholo amesema tabia hiyo hushamiri zaidi katika mashamba yaliyo mbali na makaazi ya wananchi.

“ Baya zaidi ni ile hulka ya watu hao kuiba karafuu hizo kwa kutumia njia ya kukata matawi jambo ambalo linapunguza kasi ya uzazi wa Mikarafuu iliyokatwa ”Alisema Bwana Khamis Cholo.

Amewashauri Masheha kupitia Kamati hiyo maalum kuandaa utaratibu wa uhakiki kwa watu wanaomiliki Mikarafuu vyenginevyo ni kuwachukulia hatua za kisheria wale wanaokutwa na Karafuu ambao si wakulima wala wanunuzi.

Amesema hatua hiyo itasaidia kudhibiti bidhaa hiyo muhimu ambapo wengi wa watu hao kusafirishwa kimagendo.

“ Wizi umekithiri , Wakorofi wapo na wizi wa Karafuu hivi sasa umefanywa kuwa ni jambo la kawaida tuu ”. Alifafanua Bwana Khamis Cholo.

Akizungumza Baada ya Kamati hiyo kuwahoji Baadhi ya Watu wanaojihusisha na Mashamba ya Serikali katika Skuli ya Kinyasini Wete Mwenyekiti wa Kamati hiyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewasihi Wananchi wanaomiliki eka tatu tatu ambao tayari Wazazi wao wameshafariki Kufanya utaratibu wa kuripoti katika taasisi husika ya ardhi na baadaye kujaza fomu za maombi ya kumilikishwa mashamba hayo.

Balozi Seif amesema taratibu wa umiliki wa eka tatau tatu unaeleza kwamba mtu mwenye haki ya kurithi moja kwa moja ni kati ya mke na mume kutegemea anayefariki mwanzo, wengineo wanalazimika kupeleka maombi ya kumilikishwa shamba hizo.

Akizungumzia kuhusu suala la tabia iliyojitokeza ya baadhi ya watu kusafirisha sukari nje ya nchi Balozi Seif amesema si vyema wananchi wakaendelea kuilaumu serikali moja kwa moja.

Amesema ni vizuri wananchi wakaendelea kutoa ushirikiano zaidi kuwadhibiti wakorofi hao ambao wanajaribu kutishia uhaba wa bidhaan hiyo na hatimae kuleta usumbufu kwa wananchi.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
9/9/2011.

1 comment:

  1. Hivi,ndugu zangu kwanini serekali yetu haitaki kua serious na masuala ya hizi heka? kama hizo taratibu za umiliki zipo bila shaka na rekodi za ipi alipewa nani na lini itakua zipo! hivi panafichwa nini? tena cha kushangaza wale wanaodai kua na uchungu na nchi ndio hao hao waliopewa wizara inayo husika na ardhi.Ikumbukwe,kua na uchungu na nchi sio kusema tuu au kutunisha mashavu na kukunja uso ni kujali rasilimali zake zisiharibike.

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.