Habari za Punde

KUTOKA BARAZANI - VIONGOZI WA SERIKALI WANAFANYA MAGENDO YA KARAFUU

Na Khadija Khamis-Maelezo

Baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar wamedai kuwa kuna baadhi ya viongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar wanatumia nyadhifa zao kwa kusafirisha zao la Karafuu kwa njia ya Magendo.

Wamesema kuwa kitendo hicho kinarejesha nyuma maendeleo ya nchi kwani wakulima wadogo wadogo ambao huhifadhi karafuu zao kidogo husumbuliwa na vikosi kwa kunyanganywa karafuu hizo wakati viongozi hao wajuu hawachukuliwi hatua yeyote.


Wakichangia mswaada wa Sheria Mpya ya Shirika la Biashara la Taifa Zazinbar (ZSTC) uliowasilishwa leo kwenye Baraza la Wawakilishi na Waziri wa Biashara, Viwanda, na Masoko Zanzibar Nassor Ahmed Mazrui wamesema kuwa kitendo cha kuwanyanganya wakulima wadogo karafuu zao na kuwaacha huru viongozi hao kusafirisha magendo ni ukiukwaji wa haki.

Wamesema kuwa umefika wakati kwa ZSTC kubinafsishwa ili uwepo ushindani mzuri wa kibiashara na Serikali kuondoa mkono wake katika baishara hiyo.

Wamesema kuwa ikiwa shirika la ZSTC litabinafsishwa swala la magendo litapungua kwani kila mtu atakuwa yuko macho katika kulinda mali yake.

Wajumbe hao wa Baraza la Wawakilishi wamesema kuwa hivi sasa serikali inatumia fedha nyingi katika kulinda karafuu hizo dhidi ya magendo, ambazo zingeweza kutumika katika kushughulikia mambo mengine ya maendeleo ya nchi.

Hata hivyo wajumbe hao wameipongeza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kutoa bei nzuri kwa wakulima katika kuuza karafuu hizo jambo ambalo limesaidia sana katika kupunguza magendo ya karafuu.

Wamesema kuwa mbali na hilo bei hiyo itasaidia sana katika uimarishaji wa zao hilo kwa ajili ya kuwapatia fedha za kigeni ambazo husaidia katika maendeleo ya nchi.

Mapema akiwailisha Mswaada huo mpya wa ZSTC Waziri Mazrui alisema kuwa Serikali itaandaa mikakati ya kuimarisha zao la Karafuu kwa kushugulikia matatizo yanayokwaza uzalishaji pamoja na kupunguza gharama za uendeshaji wa zao hilo.

Shirika la Bishara la ZSTC limeanzishwa chini ya Sheria ya Mashirika ya Umma ya mwaka 1960 ambapo pamoja na mambo mengine lina jukumu la kuimarisha mazao ya kilimo na uendelezaji wa masoko yake

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.