Habari za Punde

WALIOKOPA MFUKO WA JK, AK WAZINDUKA KUANZA KULIPA

HALI ya urejeshaji wa mikopo kwa wananchi waliokopeshwa kupitia mfuko wa AK na JK umeanza kuimarika baada ya kuongezeka kwa kiwango cha wanaorejesha fedha hizo.

Waziri wa Kazi, Uwezeshaji, wa Wananchi Kiuchumi na Ushirika, Haroun Ali Suleiman, aliyasema hayo jana wakati akijibu suali la Mohammed Said Mohammed (Mpendae) aliyetaka kujua ni endapo serikali ina mpango wa kuweka mfumo wa kutumia mfuko mmoja wa mikopo unaoanzisha ili kuondoa kasoro zilizojitokeza.


Waziri Haroun, alisema serikali inakubaliana na wazo hilo kutokana na hivi sasa wanajiandaa kuupitia upya mfumo wa mifuko hiyo utaokuwa unasimamia na utoaji wa mikopo na urejeshaji.

Alisema Wizara inachokifanya ni kupitia mifuko mbali mbali iliyopo hivi sasa ikiwa ni hatua ya kuangalia changamoto zake na mafanikio yalioweza kupatikana.

Waziri huyo alisema hivi sasa tayari hali ya urejeshaji wa mikopo imeonesha kuimarika kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu ambao wameanza kurejesha fedha hizo baada ya kuelimishwa madhumuni ya mikopo waliyochukua.

Alisema imeonekana ipo haja kwa serikali kuweka utaratibu mzuri wa mifuko hiyo ikiwa pamoja na kuangalia uwezekano wa kuwa na mfuko mmoja mkuu wa kuwawezesha wananchi kiuchumi.

Itachosuimamia hivi sasa Waziri huyo ni kuona serikali inasimamia urejeshaji wa mikopo ili iweze kuwanufaisha wengine.

Akitaja mikakati iliyochukuliwa na Wizara hiyo katika kufanikisha hilo waziri huyo alisema ni pamoja na kuzishajiisha Kamati za Uwezeshaji za shehia na Wilaya zifanye kazi zake kwa kufuata muongozo wa mpango wa Uwezeshaji wananchi kiuchumi.

Eneo jengine alilitaja Waziri huyo ni pamoja na kutoa elimu kwa wakopaji ili waweze kufahamu wajibu wao wa kurejesha mikopo hiyo, namna ya kusimamia biashara zao na kujua taratibu za mikopo hiyo.

Waziri huyo akiendelea alisema pia mkakati huo utawahusisha utoaji wa taaluma kwa wanasiasa wakiwemo Wabunge, Wawakilishi ikiwa ni hatua ya kuweza nao kuto mchango wa elimu ya mikopo kwa wananchi wao.

Aidha Wizara hiyo imepanga kuwafuatilia wakopaji katika maeneo yao kwa kushirikiana na masheha ikiwa pamoja na kuongeza baadhi ya vipengele katika muongozo wa usimamizi wa mikopo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.