Habari za Punde

KIKOSI CHA ZANZIBAR HEREOS NDANI YA NYUMBA DAR - CHAANZA VIBAYA CHALENJI

 Kikosi cha Timu ya Taifa ya Zanzibar, Zanzibar Heroes uwanja wa Taifa kikishiriki Chalenji.
MCHEZAJI wa timu ya taifa ya Zanzibar 'Zanzibar Heroes' Waziri Salum (kulia) akimtoka wa mlinzi wa Uganda Dan Wagaluka wakati wa pambano la michuano ya Chalenji, lililochezwa kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam jana. Uganda ilishinda 2-1.(Picha na Haroub Hussein)


Na Salum Vuai, Dar es Salaam

TIMU ya soka ya taifa ya Zanzibar 'Zanzibar Heroes', imeanza vibaya mchuano ya Kombe la Chalenji baada ya kukubali kipigo cha magoli 2-1 mbele ya Uganda Cranes, katika mchezo mkali uliochezwa uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam jana.

Zanzibar Heroes ambayo iliwahi kutwaa ubingwa wa michuano hiyo mwaka mwa 1995, ilikuwa imeweka kambi ya wiki mbili nchini Misri kujinoa na ngarambe hizo za mataifa ya Afrika Mashariki na Kati.
Ikicheza vizuri, Zanzibar Heroes ilijitahidi kutengeneza nafasi kadhaa za kupata magoli, lakini ilijikuta ikishindwa kuzitumia vizuri nafasi hizo.


Kiungo, Ali Kani kunako dakika ya 32 alipiga krosi nzuri langoni mwa Uganda iliyomkuta Ali Badri ambaye alipata kigugumizi cha miguu na mpira kuokolewa na mabeki wa Cranes.

Uganda ilijibu shambulio hilo ambapo Emanuel Okwi alipiga mpira wa hatari uliookolewa na mlinda mlango Mwadini Ali.

Baada ya mashambulizi ya kila upande, hatimaye Uganda Cranes ilifanikiwa kuandika goli la kwanza lililofungwa na Danny Wagaluka kwenye dakika ya 40, baada ya kuachia shuti kali lililomshinda mlinda mlango, Mwadini Ali, kufuatia makosa yaliofanywa na kiungo Abdulhalim Humoud.

Pamoja na kufungwa goli hilo, vijana wa Zanzibar Heroes walitulia na kufanya mashambulizi ambapo ilifanikiwa kusawazisha kunako dakika ya 46 kupitia Ali Badru ambaye hata hivyo alilazimika kutoka uwanjani baada ya kuumia kwenye dakika ya 51 na nafasi yake kuchukuliwa na Makame Hamad.

Uganda Cranes ilifanikiwa kuandika goli la ushindi katika dakika ya 77 lililofungwa na Mike Semaga, aliyesogezewa mpira mzuri na Emanuel Okwi kabla ya kuachia shuti kali la mguu wa kushoto lililojaa wavuni.
Vijana wa Zanzibar Heroes wanatarajia kujitupa uwanjani tena Novemba 27 kuvaana na Burundi.

Akizungumzia mchezo huo, Kocha wa Heroes, Abdelfatah Abbas, alisema, pamoja na kupoteza mchezo huo, bado wanayomatumaini ya kufanya vizuri katika michezo miwili iliyobakia dhidi ya Burundi na Somalia.

Hata hivyo, Mmsiri huyo alielezea kukosekana kwa baadhi ya wachezaji akiwemo Abdi Kassim na Nassor Said 'Cholo', kuliifanya timu hiyo kutokuwa vizuri zaidi katika mchezo huo.

Zanzibar Heroes imepangwa katika kundi 'B' lenye timu za Burundi, Uganda na Somalia huku kundi 'A' likiundwa na wenyeji Tanzania Bara, Rwanda, Ethiopia na Djibout.

Kundi 'C' litakuwa na timu za Sudan, Kenya, Eritrea na Malawi.
Zanzibar Heroes: Mwadini Ali, Ndir Haroub 'Canavaro', Juma Othman, Othman Omar, Aggrey Morris, Abdulhalim Humoud, Suleiman Kassim, Abdulghan Gulam, Ali Badru, Wazir Salum na Ali Kani.
Uganda: Obby Dhaira, Andrew Musigwa, Simon Musaba, Godfrey Walusumbi, Issac Baule, Danny Wagaluka, Mike Semaga, Patrick Ochan, Emanuel Okwi na Mike Mulyaba

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.