Habari za Punde

KMKM YAICHAPA NUNDU 2-0

Na Mwanajuma Juma

MAAFANDE wa KMKM wamewachezesha mchakachaka vijana wa timu ya Mundu kutoka Nungwi baada ya kuwafunga magoli 2-0, katika pambano la Ligi Kuu ya Seagull lililochezwa kwenye uwanja wa Mao Dzedong mjini hapa jana.

Pambano hilo ambalo lilianza kwa kila upande kumsoma mwenzake, lilikuwa na ushindani kiasi na kutoa burdani tosha kwa mashabiki wachache waliohudhuria uwanjani hapo.


Timu zote mbili zilionekana kucheza kwa hofu hali iliyopelekea kwenda mapumziko huku zikiwa hazijafunga.
Hata hivyo, kipindi cha pili kilianza kwa matumaini makubwa kwa KMKM ambao waliweza kupata goli la kuongoza katika dakika ya 58 kupitia kwa mchezaji wake, Juma Mbwana, ambaye alipokea pasi nzuri kutoka kwa Ame Khamis ‘Kibobea’ aliyeingia katika kipindi cha pili cha mchezo huo.

KMKM ambao walionekana kutaka ushindi katika mchezo huo, waliongeza kasi ya mashambulizi na ilipofika dakika ya 67, Mudrik Muhibu, aliiandikia goli la pili timu yake na kuwafanya waondoke uwanjani hapo wakiwa na pointi tatu.

Goli hilo lilitokana na mkwaju wa penalti baada ya Jasady Nganila wa Mundu, kumzuia Haji Simba ambaye alikuwa tayari kuziona nyavu.

Ligi hiyo itaendelea tena leo uwanjani hapo kwa mchezo utakaowakutanisha Miembeni United dhidi ya Polisi.
Naye Haji Nassor kutoka Pemba, anaripoti kuwa timu ya Chipukizi imefanikiwa kuilaza Jamhuri ya Wete goli 1-0, katika mchezo uliochezwa uwanja wa Gombani.

Goli pekee la Chipukizi katika pambano hilo lililohudhuriwa na mashabiki wengi, lilifungwa na Nassir Omar kwenye dakika ya pili kutokana na mpira wa adhabu ndogo uliokwenda moja kwa moja wavuni.

Hata hivyo, Jamhuri iliweza kupata goli ambalo lilifungwa na Mbarouk Ali kwenye dakika ya 50, lakini lilikataliwa na muamuzi wa mchezo huo.

Jamhuri ilifanikiwa kuilaza Super Falcon magoli 2-0 katika mchezo wa ufunguzi wa ligi hiyo kabla ya kusimamishwa na mahakama kutokana na shauri lililokuwa limewasilishwa na klabu ya Malindi kupinga kuenguliwa kwenye ligi hiyo.

Lakini hatimaye ligi hiyo ilianza tena juzi baada ya Malindi kushindwa kutekeleza agizo la mahakama na Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), na hivyo kuteremshwa hadi katika daraja la pili wilaya ya Mjini.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.