Habari za Punde

CCM: MNAOTUHUMIWA UFISADI IVUENI GAMBA KWA HIARI

· Chaitaka dola kutovumilia uvunjifu wa amani

Na Mwantanga Ame

KIKAO cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), kimewataka viongozi wanaotuhumiwa kwa zigo la ufisadi waanze kujitafakari, kujipima na kujichukulia hatua wenyewe kabla Chama hakijawawajibisha ikiwa ni hatua itayolinda maslahi ya chama hicho.

Hatua hiyo ya CCM imetangazwa jana na katibu Mkuu wa CCM Wilson Mkama, wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari baada ya kukamilika kwa kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ambapo hapo awali kilitanguliwa na kikao cha Kamati ya Maadili ya CCM na kikao cha Kamati Kuu.


katika kikao hicho hapo awali aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tanzania, Edward Lowasa, wakati wa kujadili ajenda ya hali ya kisiasa alilalamika kudai kushutumiwa na Katibu Mwenezi wa chama hicho Nape Nawiye kuhusika na ufisadi na kudai kuwa amekuwa akimtangazia hilo katika mikoa kadhaa ya Tanzania.

Mukama akitoa taarifa hiyo alisema CCM baada ya kuyatafsiri maazimio yake 27 ya Aprili 10-11, 2011, na kupokea taarifa ya utekelezaji wa azimio la Viongozi wa CCM wanaotuhumiwa kwa ufisadi wametakiwa kutafakari na wajipime kwa maslahi ya chama, na kujichukulia hatua wenyewe na wasipofanya hivyo, chama kiwawajibishe bila kuchelewa.

Alisema katika kutekeleza sehemu ya pili ya uamuzi huo, Halmashauri Kuu ya Taifa tayari imeiagiza Kamati Kuu pamoja na kamati za siasa za ngazi zote za chama, kupitia kamati za usalama na maadili za ngazi zao, kuanza mara moja mchakato wa kutekeleza azimio hilo.

Alisema kwa mujibu wa kanuni na taratibu zinazohusika za chama, na kwamba zoezi hilo lifanyike bila kuchelewa ikiwa ni hatua ya kukiweka sawa chama hicho kwa haraka.

Mukama alisema baada ya kukamilika kwa kazi hiyo, taarifa za utekelezaji zitapelekwe kwenye vikao vya kikatiba vya chama ili kuona namna ya kuzifanyia kazi.

Eneo jengine ambalo alilitaja Mukama, kikao hicho kimeamua kufanyiwa kazi linalohusu vurugu zinazoendelea kutokea katika miji ukiwemo wa Arusha, Mwanza na Mbeya ambapo imeitaka dola kuchukua hatua thabiti na za haraka kudhibiti vitendo vya hujuma na uharibifu kwa mali za Watanzania.

Alisema halmashauri Kuu imesisitiza kuwa kusiwepo kabisa na uvumilivu kwenye uvunjaji wa amani kwa kisingizio cha kudai haki na Viongozi wa vyama vya siasa wanaojihusisha na vitendo vya uchochezi na hujuma wachukuliwe hatua za kisheria bila kuogopwa.

Alisema hivi sasa kumejitokeza wimbi la vurugu katika maeneo mbalimbali hapa nchini, hasa katika Majiji ambayo hivi karibuni yameripotiwa kutokea vurugu zikifanywa zaidi na vijana wa Mwanza, Mbeya na Arusha ambapo serikali imetaka kudhibitiwa.

Hata hivyo Katibu huyo alisema katika kukabiliana na hali hiyo Halmashauri Kuu ya Taifa imeitaka Serikali kuharakisha kutatua matatizo yanayowakabili vijana wa mijini, hususan tatizo la ajira na maeneo ya kufanyia biashara zao ndogo ndogo.

Pia Mukama alisema serikali imetakiwa kuuangalia upya mfumo wa elimu nchini ili vijana wengi wanaomaliza darasa la saba na kidato cha nne wawe na stadi za ufundi zitakazowapa uwezo wa kujiajiri na kuajiriwa na kutekeleza mpango wa kujenga skuli za ufundi kwenye kila wilaya uliomo kwenye llani ya Uchaguzi ya CCM ya 2010-2015 utekelezwe kwa haraka.

Akiendelea katibu huyo alisema kuhusu suala la mjadala wa Katiba, kikao hicho cha Halmashauri Kuu ya Taifa kimewataka wananchi na wanachama wa CCM kuelewa, kutambua, na kuamini kwamba Katiba mpya pamoja na mchakato wa kuipata, upo kwa manufaa ya nchi na Wabunge na viongozi wengine wa ngazi zote nchi nzima wanapashwa kuwaelewesha wananchi si tu maudhui yake, bali hata faida zake.


Alisema katika kutekeleza hilo kikao hicho kimeiagiza Serikali, pamoja kupitia Tume ya Kukusanya Maoni, iweke msukumo wa kutoa elimu kwa umma wakati wote kuhusu jambo hilo na mchakato mzima ili kuzuia upotoshaji unaofanywa kwa wananchi kuhusu mchakato mzima wa kupata Katiba mpya.


Amesema imeitaka Serikali ihakikishe hakuna Chama chochote cha siasa, mtu, kikundi cha watu au taasisi yoyote ikayotumia mchakato wa kupata Katiba mpya kuchochea vurugu na uvunjifu wa amani.

Vyombo vya Usalama alisema katika kusimamia suala hilo navyo vitatakiwa viwe imara katika kuhakikisha kwamba Sheria za nchi zinafuatwa na wanaochochea vurugu wanachukuliwa hatua kali bila kujali nafasi zao.

Aidha, alisema Kikao hicho kinampongeza Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete kwa hotuba yake aliyoitoa kwa wazee wa Dar es Salaam kwa ufafanuzi na maelezo fasaha kwa mambo makubwa na ya msingi yanayolikabili taifa hilo hivi sasa.

Kuhusu sakata la katibu Mkuu wa Nishati na Madini David Jairo, Mkama alisema kikao hicho cha Halmashauri Kuu,


Kuhusu Migogoro katika Vyuo vikuu na taasisi za Elimu ya Juu mkama, alisema Halmashauri Kuu ya Taifa imeitaka Serikali ihimize utawala bora katika menejimenti za baadhi ya vyuo vikuu vya umma ikiwa ni hatua ya kusaidia jawabu la kupunguza malalamiko, migogoro, migomo na vurugu katika baadhi ya vyuo.


Aidha, alisema halmashauri hiyo pia imeitaka Serikali kutekeleza Sheria yake ya kupiga marufuku harakati za siasa na uvaaji wa sare za vyama katika maeneo ya vyuo (Campuses) na wafanyakazi wa vyuo na wanavyuo wanaopenda kujihusisha na harakati za siasa basi wafanye hivyo nje ya maeneo ya vyuo ikiwa ni hatua ya itayo ifanya jamii ya wanavyuo kutoingilia shughuli za masomo na mipango ya vyuo.


Hata hivyo, Mkama alisema Kikao hicho kimeiagiza Serikali kuendelea kufuatilia kwa karibu hali ya migogoro na malalamiko hasa katika Chuo Kikuu cha Dodoma na ichukue hatua muafaka kurekebisha hali hiyo.

Kuhusu sakata Halmashauri Kuu ya Taifa alisema imeipongeza Serikali kwa uamuzi wake wa kuipokea taarifa ya Kamati Teule ya Bunge na kuahidi kuifanyia kazi na inaipongeza Serikali kwa uamuzi wake wa kuipokea taarifa ya Kamati Teule ya Bunge na kuahidi kuifanyia kazi.


Kutokana na maafa yaliyotokea Septemba 10, 2011 ya kuzama kwa meli ya Spice Islander I, Mukama alisema Halmashauri Kuu ya Taifa imezipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa hatua thabiti na za haraka ilizochukua katika kipindi chote cha maafa na msiba huo na hata baada.


Alisema inawapongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein kwa kutoa miongozo thabiti na kuongoza katika kuwafariji na kuwatuliza wananchi wa visiwa vya Zanzibari na Watanzania kwa jumla katika kipindi chote cha msiba huo.


Pia Halmashauri Kuu ya Taifa, imewashukuru watu binafsi na taasisi mbalimbali zilizoshiriki kwenye zoezi la uokoaji na zilizochangia kwa hali na mali, kwa fedha na vifaa, katika msiba huu na inawashukuru na kuwapongeza wananchi wa visiwa vya Unguja na Pemba waliojitolea kushiriki kwenye zoezi la uokoaji.

“Kwa kuwa tayari Tume imeundwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti Baraza la Mapinduzi, Halmashauri Kuu ya Taifa imewataka wananchi wasubiri na waiache ifanye kazi yake kwa uadilifu na kwa muda uliopangwa na kuhakikisha kuwa mapendekezo ya tume hiyo yanafanyiwa kazi” Alisema Mkama.

Hata hivyo, alisema Halmashauri hiyo imeiagiza pia Serikali kuendelea na jitihada zake za kurahisisha usafiri wa abiria kati ya Unguja na Pemba na kati ya visiwa hivyo na Tanzania Bara ikiwa pamoja na kutekeleza nia yake ya kununua meli zake.

Kuhusu suala la chakula nchini alisema kikao hicho kimeitaka Serikali iimarishe Wakala wa Chakula wa Taifa kwa kuuwezesha kwa fedha zaidi na kujenga maghala mengi na makubwa zaidi ili uweze kununua kiasi kikubwa cha mazao.


Mukama alisema pia kikao hicho kimeiagiza Serikali ihimize kuundwa kwa Vyama vya Ushirika vya Mazao ya Chakula, ambavyo navyo viwezeshwe kujenga maghala ya kuhifadhi nafaka katika maeneo yao pamoja na kuanzisha mfumo wa ununuzi wa mazao wa stakabadhi ghalani.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.