Habari za Punde

Dkt. Salem Al-Junaibi na Ujumbe wake Uwewasili Nchini kwa Ziara ya Kibiashara

 

Mwenyekiti wa Chama cha Biashara na Viwanda cha Oman Dkt. Salem Al-Junaibi (Mb) na ujumbe wa Wafanyabiashara wa Oman, amewasili nchini leo, tarehe 7 Septemba 2025, kwa ziara ya siku tano, kuangazia fursa za uwekezaji na biashara za Tanzania, katika sekta mbalimbali.

Mara baada ya kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dkt. Al-Junaibi na ujumbe wake, alipokelewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Twaibu, pamoja na Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Abdalah Kilima. 

Viongozi wengine waliompokea ni Naibu Balozi wa Oman nchini Tanzania, Rashid Al Mandhir, pamoja na maafisa waandamizi wa Serikali na Sekta binafsi.

Katika ziara yao, Dkt. Al-Junaibi na ujumbe wake wanatarajiwa kukutana na viongozi wa Serikali pamoja na taasisi mbalimbali za umma na binafsi, zikiwemo Tume ya Ushindani (FCC), Kiwanda cha Nyama – Kibaha, Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA), KAMAKA, TISEZA, BRELA, TANTRADE, TBS, TIRDO na Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC).

Aidha, ujumbe huo pia utatembelea Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Wakala wa Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), pamoja na Bodi ya Chai Tanzania (TTB). 

Vilevile ujumbe huo pia utashiriki katika mazungumzo na Makatibu Wakuu wa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Nishati, pamoja na Ofisi ya Rais – Kazi, Uchumi na Uwekezaji. Katika mikutano hiyo, pande hizo mbili pia zitasaini mikataba mbalimbali ya ushirikiano kati ya Tanzania na Oman.

Dkt. Al-Junaibi na ujumbe wake pia watatembelea Zanzibar ambako watakutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa ZIPA, ZNCC, pamoja na kutembelea Eneo Maalum la Uchumi Zanzibar.

Mbali na mazungumzo hayo na Serikali ya Tanzania Bara na Zanzibar, ujumbe huo wa wafanyabiashara wa Oman pia utafanya mawasilisho kuhusu hali ya biashara na viwanda nchini Oman, pamoja na fursa mbalimbali za ushirikiano wa kibiashara kati ya Oman na Tanzania.

Ziara hiyo ya Dkt. Al-Junaibi na ujumbe wake inatarajiwa kukamilika tarehe 12 Septemba, 2025, kabla ya kurejea nchini Oman.











No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.