Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein,akizungumza na Balozi wa Jumuiya ya Ulaya Tim Clarke alipofika Ikulu Mjini Zanzibar kumuaga Rais baada ya kumaliza muda wake wa kazi nchini.
Picha na Ramadhan Othman IKULU
Na Rajab Mkasaba, Ikulu
JUMUIYA ya Ulaya (EU), imeeleza azma yake ya kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha na kuendeleza miradi mbali mbali ya maendeleo huku ikieleza lengo la kuwa na afisi zake hapa Zanzibar.
Balozi wa Jumuiya EU, anaemaliza muda wake wa kazi nchini Tanzania, Tim Clarke, alieleza hayo jana alipokuwa na mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, Ikulu mjini Zanzibar.
Balozi Clarke alimueleza Dk. Shein kuwa Jumuiya ya Ulaya imeona haja ya kuanzisha afisi zake hapa Zanzibar kwani pia, itarahisisha utendaji wa kazi wa Jumuiya hiyo hapa Zanzibar.
Balozi huyo alitoa pongezi kwa mafanikio makubwa yaliyofikiwa Zanzibar chini ya uongozi wa Rais Dk. Shein.
Alieleza kuwa Jumuiya ya Ulaya inajivunia mafanikio yaliyofikiwa Zanzibar na kueleza kuwa juhudi zitaendelea kuchukuliwa katika kuendeleza miradi ya maendeleo kwa upande wa Unguja na Pemba.
Pia, Clarke alieleza kuwa Jumuiya ya Ulaya itaendelea kuunga mkono juhudi za serikali katika kukuza na kuendeleza utamaduni, sambamba na kuutangaza utamaduni huo kupitia matamasha.
Nae Dk. Shein alitoa pongezi kwa Jumuiya ya Ulaya na kueleza kuwa Zanzibar inathamini sana juhudi zinazochukuliwa na jumuiya hiyo katika kuunga mkono uimarishaji wa sekta za maendeleo hapa nchini.
Dk. Shein alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inaunga mkono azma ya Jumuiya hiyo ya kuanzisha afisi zake hapa Zanzibar.
Aidha, Dk. Shein alieleza kuwa Jumuiya ya Ulaya imeweza kusaidia miradi mbali mbali hapa Zanzibar ambayo imeweza kuleta mafanikio makubwa.
Alieleza kuwa pamoja na hatua hizo, wananchi wa Zanzibar wanaendelea kuishi kwa amani na utulivu.
Alieleza kuwa wananchi wa Zanzibar wameonesha msimamo wao mkubwa katika kuhakikisha wote ni wamoja na wana jukumu la kujenga nchi yao kwa maendeleo yao na nchi yao kwa jumla.
Sambamba na hayo, Dk. Shein alipongeza lengo la Umoja wa Ulaya kuanzisha afisi zake hapa Zanzibar na kueleza kuwa hatua hiyo itasaidia kurahisisha utekelezaji washughuli za EU kwa Zanzibar.
Wakati huo huo Dk. Shein alitembelea eneo la Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) huko Tunguu, wilaya ya Magharibi Mkoa wa Kusini Unguja kuangalia hatua za ujenzi wa majengo ya chuo hicho zinavyoendelea.
Dk. Shein alitembelea na kuona hatua hizo za ujenzi pamoja na kupata maelezo kutoka kwa wataalamu wa ujenzi kutoka kampuni ya ujenzi ya Masasi inayoendelea na ujenzi wa majengo ya chuo hicho.
Kwa mujibu wa maelezo ya uongozi wa Kampuni ya Masasi, ujenzi huo wa majengo ya chuo hicho ambayo baadhi yake yamefikia hatua nzuri unatarajiwa kukamilika mwezi Machi mwakani.
Katika ziara hiyo Dk. Shein pia, alitembelea na kuangalia mipaka ya eneo la chuo hicho huku akisisitiza haja ya kulihifadhi na kulilinda ili kuepuka kuvamiwa.
Sambamba na hayo, uongozi wa Mkoa wa Kusini Unguja kupitia Halmashauri yake ya wilaya ya Kati iliendelea kusisitiza kuwa wale wote waliovamia katika eneo hilo la chuo kwa kujenga nyumba za kuishi ambao tayari wameshapewa amri ya kuhama wametakiwa kufanya hivyo mara moja.
No comments:
Post a Comment