Ni za kuchapuza shughuli za maendeleo
Waziri, Balozi wapongeza ushirikiano
Na Mwantanga Ame
SERIKALI ya Zanzibar imeanza kufaidika na utekelezaji ahadi ya serikali ya China ya kusaidia maendeleo ya wananchi wa Zanzibar baada ya kuipatia zaidi ya shilingi bilioni 12.8.
China imetoa fedha hizo baada ya kuweka saini mkataba utaoiwezesha Zanzibar kupata fedha kwa ajili ya shughuli za maendeleo kwa kila mwaka kutoka serikali ya China.
Hatua ya China kuweka saini mkataba huo inakuja ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi iliyoitoa kwa serikali ya Zanzibar wakati Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi alipofanya ziara nchini humo.
Kutokana na ahadi hiyo Balozi wa China nchini Tanzania, Liu Kinsheng, jana asubuhuhi aliweka saini mkataba huo na waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha, Uchumi, Mipango ya Maendeleo, Omar Yussuf Mzee, alitia
saini kwa niaba ya serikali ya Mapinduzi.
Balozi Kinsheng alisema katika mkataba huo, China itaipatia Zanzibar Yuani milioni 50, ambazo ni sawa na dola za Marekani milioni 8, ambazo matumizi yake yatapangwa na serikali ya Zanzibar kwa kuyalenga maeneo ya maendeleo kwa ajili ya wananchi wa Zanzibar.
Alisema China itaendelea kutoa misaada yake kwa Zanzibar kutokana na kutambua umuhimu wa kuwasaidia wananchi, kwa kuyaangalia maeneo mapya ya kiuchumi.
Alisema hiyo inatokana na kuwa Zanzibar imekuwa na urafiki wa muda mrefu na serikali ya China na wanalazimika kuongeza ushirikiano ili serikali iweze kupiga hatua zaidi.
Balozi huyo alisema ingawa serikali hiyo imetoa fedha hizo lakini matumizi yake yatapangwa na serikali ya Zanzibar kwani wanafahamu kuwa hivi sasa kuna maeneo ambayo yanahitaji kupatiwa msaada ili yaweze
kufanya vizuri.
Akiyataja maeno hayo ni pamoja na yanayohusu huduma za kijamii, shughuli za kilimo, viwanda na ukuzaji manzingira ya utoaji wa elimu.
Alisema hivi sasa China imekuwa ikitekeleza mradi wa ujenzi wa jengo la pili la kupumzikia wageni katika kiwanja cha Ndege cha Zanzibar, mradi ambao umeongeza ushirikiano kwa pande zote mbili.
Mapema waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha, Uchumi, Mipango ya Maendeleo, Omar Yussuf Mzee, akitoa maelezo alisema serikali inafarajika na hatua ya serikali ya China katika kusaidia maendeleo ya
Wazanzibari.
Alisema hiyo inatokana na historia iliyopo kwa taifa hilo la China limekuwa lina urafiki mkubwa na serikali ya Zanzibar pamoja na mapenzi na wananchi wa Zanzibar katika kuwakwamua katika hali ya umasikini.
Alifahamisha kuwa serikali imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbali mbali ambazo zinazohitaji kufanyiwa kazi, ambapo msaada huo utasaidia kukabiliana na changamoto hizo.
Akizitaja Changamoto hizo alisema ni pamoja na tatizo la maji katika maeneo mbali mbali ya mjini, ukosefu wa madawati katika skuli za serikali na maeneo mengine ya huduma za kijamii.
Nae Kamishna wa Fedha za Nje Zanzibar, Saada Mkuya, akitoa shukrani kwa Balozi huyo, alisema serikali itaendelea kuithamini misaada inayotolewa na China kwani imekuwa na mchango mkubwa wa kusukuma mbele hatua za kimaendeleo.
Akitaja misaada ambayo China imekuwa ikiisaidia Zanzibar ni pamoja na ujenzi wa skuli ya kisasa ya Mwanakwerekwe, ujenzi wa jengo la Redio Zanzibar na fedha hizo pia zitasaidia katika uwekaji wa taa za
barabarani katika Mji wa Zanzibar.
Utiaji saini huo ulishuhudiwa na Balozi mdogo wa China aliyepo Zanzibar, Chen Quiman na maofisa wengine wa ubalozi wa Dar es Salaam na Zanzibar na baadhi ya makamishna wa wizara ya Fedha.
No comments:
Post a Comment