Habari za Punde

MAOFISA MIPANGO WATAKIWA KUZINGATIA IDADI YA WATU

Na Madina Issa

KATIKA kukabiliana na changamoto ya ongezeko ya idadi ya watu visiwani Zanzibar, ipo haja ya kutoa taaluma kwa wananchi ili waweze kwenda sambamba na mabadiliko ya kiuchumi yanayotokea duniani.

Akifungua katika mkutano wa uwasilishaji ripoti ya mwaka 2011 juu ya masuala ya idadi ya watu Zanzibar kwa maofisa Mipango wa mawizara, mikoa, wilaya, halmashauri na taasisi mbali mbali, Kamishna Idara ya
Mipango na Maendeleo ya Watenda Kazi wizara ya fedha, Seif Shaaban Mwinyi alisema maofisa hao wananajukumu katika kuhakikisha watumishi wa taasisi zao wanakuwa na taaluma katika kuiendeleza nchi kiuchumi.


Kamishna huyo alisema licha ya ongezeko hilo la idadi ya watu katika visiwa vya Zanzibar, bado kuna fursa ya kuweza kuendelea kiuchumi endapo wananchi wake wataelimishwa katika masuala ya maendeleo.

“Endapo watu waliopo watakuwa wenye ubora na sio bora watu, walioelimishwa vizuri, wenye uwezo mzuri wa uzalishaji na wenye uwezo mkubwa wa manunuzi katika soko (high purchasing power), basi watu hawa
licha ya wingi wao hawatakuwa mzigo katika nchi na hawatakua na athari mbaya kijamii, kiuchumi na kimaendeleo”, alisema Kamishna Seif.

Kamishna huyo aliwashauri maofisa mipango hao kulitizama suala la idadi ya watu kuwa ni jambo la msingi na la umuhimu katika mipango ya kimaendeleo kwani kila mipango inakuwa ina mlenga maendeleo yao.

Hivyo waliwasisitiza maofisa hao kuwa mipango itayowasilishwa katika taasisi zao kuhakikisha wanaifanyia kazi kivitendo kwani inakuwa na tija kwa wananchi.


Seif alifahamisha kuwa kuna baadhi ya watu wanapofanyiwa mafunzo huwa yanaishia madarasani huku makabrasha yakibakia katika makabati ya ofisini bila ya kuyafanyia kazi.

"Baadhi ya watu wanaofanyiwa mafunzo hayo hawayafanyii kazi na kuziacha ripoti zinaliwa na wadudu, tukiendekeza hivyo tutakuwa hatufikii lengo lililokusudiwa, tubadilike ili tufikie malengo yaliyokusudiwa”, aliwasisitiza.

Hata hivyo aliwashukuru waandaaji wa mafunzo hayo shirika la UNFPA kupitia UNDAP kwa msaada ulioweza kuwasilishaji wa ripoti.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.