Na Haji Nassor, Pemba
KLABU za Unguja, zimeendelea kusulubiwa na timu za Pemba katika ligi kuu ya soka Zanzibar, baada ya juzi Zimamoto kuchapwa mabao 3-2 na Jamhuri kwenye uwanja wa Gombani.
Jamhuri ambayo katika mchezo uliopita iliifyeka Mafunzo kwa goli 1-0, juzi ilionesha mapema dhamira ya kuendeleza umwamba, pale ilipoweza kuzichana nyavu za Zimamoto mnamo dakika ya sita, kwa bao la Bakari Khamis aliyeunganisha vyema krosi ya Hussein Omar.
Kama haitoshi, Jamhuri ilizihujumu tena nyavu za Zimamoto kupitia kwa Ali Othman, matokeo yaliyodumu hadi wakati wa mapumziko.
Jamhuri ilizidi kuliandama lango la wageni wao kwa nguvu, na kufanikiwa kuongeza bao la tatu, mara hii likifungwa na nahodha wake Hussein Omar katika dakika ya 57.
Hata hivyo, dakika kumi baadae, Zimamoto ilianza kuzinduka na kujifariji kwa goli la kwanza lililonasishwa nyavuni na Hakim Khamis, kabla Abdulhamid Ali kufunga la pili mnamo dakika ya 89.
Matokeo hayo yameifanya Jamhuri kujiongezea akiba yake ya pointi ambapo sasa zimefikisha kumi.
No comments:
Post a Comment