Habari za Punde

POLISI WAMSHIKILIA MMOJA KWA MAUAJI

Na Mwanajuma Said

JESHI la Polisi Mkoa wa Kusini Unguja, linamshilikilia kijana wa miaka 30 kwa tuhuma za mauaji.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Kamanda wa polisi Mkoa huo, Augustino Ollomi alimtaja mtuhumiwa huyo ni Mussa Ali, Mkaazi wa Fuoni, Wilaya ya Magharibi Unguja.

Kamanda Ollomi alifahamisha kuwa mtu huyo anatuhumiwa kumuuwa Andrea Andriano kwa kumchoma kisu sehemu ya kifuani na tumboni.


Tukio hilo limetokea Disemba 11 saa 1:30 usiku baada ya kuzuka ugomvi kwenye kilabu cha pombe, kati ya marehemu na Mussa ambapo ugomvi wao ulianzia kwenye nyumba za uuzwaji wa pombe na wote wadaiwa walikuwa tayari wamelewa.

Alisema baada ya ugomvi huo, ndipo mtuhumiwa alipoanza kumshambulia marehemu kwa kisu na kusababisha kifo chake.

"Kabla ya tukio hilo, mtuhumiwa na marehemu walizozana kwenye nyumba za kuuzia pombe na wote walikuwa wamelewa ugomvi wao uliendelea na kupelekea kutokea kifo hicho,"alieleza Kamanda Ollomi.

Kamanda Ollomi alisema baada ya tukio hilo, mtuhumiwa alitoroka na polisi walifanikiwa kumtia mbaroni baada ya kutolewa taarifa na raia wema mahali alipojificha.

"Baada ya kufanya mauaji hayo mtuhumiwa alikimbia na kujificha nyumbani kwa baba ake huko Fuoni lakini tulimtia mabaroni kwa kushirikiana na raia wema,"alifahamisha Kamanda.

Kamanda Ollomi alisema chanzo cha mauaji hayo ni utumiaji wa pombe hivyo alisisitiza wananchi kuachana na biashara hiyo kwani husababisha maafa makubwa kwa jamii.

Wakati huo huo, mtoto mdogo mwenye umri wa miaka 15 amefariki dunia baada ya kuzama kwenye shimo lililojaa maji huko Mwera Mvumoni na kumtaja marehemu kuwa Ali Kassim Khamis, mkaazi wa Mwera Unguja.

Akithibitisha kutokea kwa ajali hiyo, Kamanda Ollomi alisema marehemu alifariki majira ya saa 4:00 asubuhi ya Disemba 12 wakati alipokwenda eneo hilo na wenzake kwa ajili ya kukoga na katika jitihada za
kumtafuta alipatikana akiwa tayari ameshafariki.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.