Habari za Punde

SERIKALI ITAFANYA JUHUDI KUPUNGUZA AJALI ZA BARABARANI - DK SHEIN

Na Rajab Mkasaba

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa serikali anayoingoza itachukua juhudi katika kuhakikisha ajali za barabarani zinapungua huku akisisitiza kutowafumbia macho wanaozivunja sheria za barabarani kwani twakimu za ajali za barabarani zinatisha.

Dk. Shein alaiyasema hayo leo katika uzinduzi wa miaka kumi ya UsalamPublish Posta Barabarani, hafla iliyofanyika katika ukumbi wa hoteli ya Bwawani mjini Zanzibar na kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali akiwemo Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad.


Katika maelezo yake Dk. Shein alisema takwimu za ajali barabarani kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Zanzibar zinaonesha kuwa katika kipindi cha 2008 hadi Machi, 2011, jumla ya ajali 2,568 zilitokea na kusababisha vifo 341 na majeruhi 3,303 Unguja na Pemba.

Alisema kuwa hizo ni ajali nyingi ikilinganishwa na idadi ya watu wa Zanzibar hivyo haiwezekani hali hiyo ikaendelea ni lazima hatua za makusudi zichukuliwe ili kupunguza ajali za barabarani.

Dk. Shein alisema kuwa ajali za barabarani zinashika nafasi ya pili kwa kusababisha vifo vingi baada ya ukimwi, hasa kwa watu wenye umri wa kuanzia miaka 5 hadi 29 na pia, ni ya tatu kwa watu wenye umri wa miaka 30-44 kwa kusababisha vifo vingi baada ya ukimwi.

Dk. Shein alisema kuwa ni kweli kwamba vyombo vya barabarani vimezidi kutokana na hali ya maendeleo ya nchi, lakini pia, ni kweli kwamba kumekuwepo uzembe wa kutojali sheria kiasi kikubwa na kusisitiza kuwa serikali itaimarisha mambo matatu likiwemo uhandisi au ufundi, utiliaji mkazo sheria na elimu kwa jamii juu ya usalama barabarani.

Alieleza kuwa kwa upande wa uhandisi serikali itaendelea na ujenzi wa barabara kwa Unguja na Pemba anaozingatia watumiaji wote wakiwemo waendeshaji wa vyombo vya moto na baskeli, watembeaji kwa miguu na wale wenye mahitaji maalum ambapo ndani ya miaka mitano ijayo tatizo la barabara litamalizika.

Aidha, alisema kuwa kutahakikishwa ukaguzi wa vyombo vya moto unafanyika na kuhakikisha kuwa gari mbovu haziendeshwi barabarani na kulitaka Jeshi la Polisi pamoja na Wizara ya Miundombinu kulisimamia hilo.

Kuhusu elimu ya usalama barabarani, Dk. Shein alieleza kuwa elimu hiyo itatolewa katika skuli za msingi na sekondari ili vijana ambao ndio mabalozi wa miaka kumi ya usalama barabarabi waweze kupata elimu ya kutosha na kuiagiza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano pamoja na Jeshi la Polisi kusimamia suala hilo.

Mapema Waziri wa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano Hamad Masoud alieleza kuwa Wizara yake itahakikisha inaweka mikakati madhubuti katika kupambana na ajali barabarani ikiwa ni pamoja na kuanzisha Kitengo cha Utunzaji Endelevu wa barabara pamoja na kurekebisha sheria na kanuni za barabarani kwani zimepitwa na wakati.

Aidha, Waziri huyo alieleza haja kwa wananchi wa Zanzibar kubadilika katika matumizi mazima ya barabara ili kuweza kupunguza ajali zisizo za lazima.

Nae Mtaalamu kutoka Serikali ya Oman Dk. Wahid Alharusi, akitoa mifano ya ajali mbali mbali nchini zilizotokea nchini mwake alieleza haja ya kuimarisha miundombinu ya barabara hapa nchini pamoja na kushirikiana katika kupiga vita ajali za barabarani.

Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Afya Malick Abdalla Juma, alieleza kuwa miongoni mwa juhudi zitakazochukuliwa na Wizara yake ni pamoja na kufundisha jinsi ya kutoa huduma ya kwanza kwa jamii juu ya ajali za barabarani.

Nayo taarifa ya Kamishna wa Polisi Zanzibar ilitolewa na kuonesha takwimu za ajali za barabarani na kueleza kuwa katika kipindi cha Januari hadi Oktoba 2011, jumla ya matukio 657 ya ajali za barabarani yameripotiwa katika vituo vya Polisi hapa Zanzibar.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa miongoni mwa vyanzo vya ajali ni pamoja na ubovu wa vyombo vinavyotumia barabara, ubovu wa barabara, kukosekana kwa alama za barabani, kutojulikana kwan sheria za usalama barabarani, ulevi, ujuzi mdogo wa kuendesha gari na kuendesha gari kwa mwendo wa kasi.

Kutokana na hali hiyo Jeshi la Polisi limeeleza azma yake ya kuendelea kutoa elimu kwa jamii, kuanzisha chuo cha kufundishia madereva katika chuo cha Polisi ili kupata madereva wazuri kuhimiza doria za barabarani pamoja na mikakati mengineyo.

Marabaada ya uzinduzi huo Dk. Shein aliongoza matembezi ya kuunga utekelezaji wa miaka kumi ya usalama barabani yaliyoanzia Hoteli ya Bwawani hadi Hospitali Kuu ya MnaziMmoja ambapo pia, alipata fursa ya kuwaangalia wagonjwa wa ajali za barabarani na hatimae kuwaombea dua iliyosoma na Katibu wa Mufti Sheikh Fadhil Soraga.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.