Na Mwandishi wetu
MKURUGENZI wa vitambulisho vya Taifa (NIDA) Zanzibar, Vuai Mussa Suleiman amesema vitambulisho hivyo, vitamuwezesha kila Mtanzania kupata haki sambamba na kulindwa kwa haki hizo.
Mkurugenzi huyo alieleza hayo jana Kilimani mjini hapa, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, wakati akitoa tathmini ya zoezi la majaribio la uandikishi wa utoaji wa vitambulisho vya taifa.
Alisema umefika wakati kwa Watanzania kuwa na vitambulisho vya taifa, kwani ni fursa muhimu ya kusaidia kulinda na kuzipata haki zao.
Mkurugenzi huyo alisema vitambulisho vipya ambavyo kwa mara ya kwanza vitatoka mwezi Aprili mwakani, vitatumia teknolojia ya kisasa ili kuepuka kuvuja habari binafasi kwa wasiohitajika.
“Kitambulisho kitatumia ‘smart card’, tunaamini teknolojia ya kisasa ambayo haitaweza kuvujisha habari binafsi kwa wasiohitajika”,alisema Mkurugenzi huyo.
Alifahamisha kuwa zeozi linaloendelea hivi sasa ni la uandikishaji wa majaribio kwa wafanyakazi wa umma kwa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na serikali ya Muungano.
Alifahamisha kuwa kwa Zanzibar wanatarajia kuandikisha watumishi 32,000 kwa Unguja na Pemba ambapo kwa siku moja maofisa wa Idara hiyo Zanzibar wamekuwa wakiandikisha watumishi kati ya 800 hadi 1000.
“Kwa idadi hii wafanyakazi wamekuwa wakijitokeza sana, kwa kuelewa hilo tumewapeleka waandikishaji wetu karibu na maeneo ya kazi ili kuepuka kutumia muda mwingi kwenye uandikishaji na kukosa kutekeleza
majukumu yao”,alisema.
Aidha aliwaomba wafanyakazi kuhakikisha wanatumia fursa hiyo ya kujiandikisha ili waweze kupatiwa vitambulisho hivyo.
Katika hatua nyengine Mkurugenzi huyo alisema masheha hawaruhusiwi kupokea fedha kwa ajili ya kutia saini ya dodoso la kitambulisho hicho.
“Masheha tuliwafanyia semina, wanajua kuwa hawapaswi kuomba fedha kwa njia yeyote na kufanya hivyo ni kinyume na sheria”,alisema.
No comments:
Post a Comment