Na Donisya Thomas
KLABU ya Azam FC iliyotwaa ubingwa wa Kombe la Mapinduzi mwaka 2012, imejigamba kuwa itawafumba midomo wale wanaoibeza, wakidai mara nyingi ushindi wa timu hiyo ni wa kubahatisha, huku ikishindwa kutamba katika ligi kuu ya Tanzania Bara.
Ofisa habari wa klabu hiyo Jaffar Iddi, amesema kama ushindi wao ni wa kubahatisha, iweje klabu hiyo isiyo na muda mrefu katika soka la Tanzania imekuwa ikizisumbua mno klabu kubwa nchini zikiwemo Simba na
Yanga.
Jaffar alifahamisha kuwa wale wanaoikejeli timu hiyo, wasubiri kuona maajabu katika mzunguko wa pili ulioanza mwishoni mwa wiki iliyopita, kwani wamepania kuzitesa tena klabu hizo na hatimaye kunyakua taji la
ligi kuu.
"Nawashangaa mno wanaosema ushindi wetu ni wa kubahatisha, wanasahau kuwa tumeifunga Yanga mara mbili katika mechi ya kirafiki na michuanoya Mapinduzi, pia tukaichapa Simba katika michuano hiyo hiyo, je huko kote ni kubahatisha?" alihoji msemaji huyo.
Aidha alieleza haoni sababu kwa timu inayoshinda kwa bahati, itawazwe ubingwa wa Kombe la Mapinduzi bila ya kupoteza hata mchezo mmoja.
Jaffar alisema wale wote wanaotoa madai hayo si watu wanaoitakia mema timu hiyo hasa kutokana na kandanda safi wanalolionesha, na kuongeza kuwa mafanikio wanayoyapata yamesaidia kuwafichua mahasidi wa matajiri hao wa 'ice cream'.
No comments:
Post a Comment