• Ni kwa kuwatimua madaktari Muhimbili
Na Kunze Mswanyama, Dar
CHAMA cha Madaktari Tanzania (MAT), kimesema serikali itabeba jukumu la athari na madhara yoyote yanayolikumba taifa kufuatia maamuzi yake ya kuwatimua kazi madaktari waliokuwa wakifanyakazi katika hospitali ya taifa ya Muhimbili.
Hivi karibuni serikali iliwafukuza kazi madakatari kadhaa wanafunzi katika hospitali hiyo walioitisha na kujiunga na mgomo wa kushindikiza kulipwa posho yao ya miezi miwili.
Akizungumza nje ya ukumbi wa mkutano unaowashirikisha madaktari jijini Dar es Salaam, Makamu wa Rais wa MAT, Primusi Saidia serikali itapaswa iwajibike kutoka na madhara yatakayojitokeza kwa wagonjwa kukosa matibabu kutokana na madaktari hao kufukuzwa.
Makamu huyo alisema inasikitisha kuiona serikali ikichukua uamuzi mgumu kama huo, hali inayoleta tafsiri ya kutowajali na kuwapenda wananchi wake hasa wale wanaosumbuka na maradhi mbali mbali wakihitaji
utibabu na ushauri wa wataalamu hao.
Alisema maamuzi hao yanaonesha jinsi gani serikali inavyochezea maisha wananchi wake na kuonesha kutowajali.
Hata hivyo alisisitiza kuwa wao hawapendi kuiona hali hiyo ikijitokeza kwani kwa mujibu wa mwongozo wa udaktari ni moja kati ya kada zinazotakiwa kupewa nyumba sawa na majeshi ya ulinzi na usalama.
“Tunamtaka waziri wa Afya Dk.Hadji Mponda aje hapa na Katibu Mkuu wake kutuambia ni kwa nini analichezea taifa hivyo. Hatutaki matamko ya kwenye vyombo vya habari tunataka aje hapa kama alivyosema kuwa yupo tayari kuitikia wito wetu”,alisema Makamu huyo.
Mkutano huo ulimchagua Makamu huyo kwenda wizarani na kumchukua waziri Mponda kumpeleka kwenye ukumbi wa mkutano huo kujibu hoja zao.
Madaktari zaidi ya 250, jana waliamua kuacha shughuli zao zote za kuokoa maisha ya watu na kwenda kuitikia wito wa na chama chao ambapo kwa pamoja wanasubiri ujio wa waziri huyo ili kutoa msimamo wa
serikali juu ya mustakabali wa madaktari hao.
No comments:
Post a Comment