Habari za Punde

Raza Achukuwa Fomu ZEC Uchaguzi Uzini

Na Ramadhan Makame

MGOMBEA wa Chama cha Mapinduzi kwenye uchaguzi mdogo wa jimbo la Uzini, Mohammed Raza jana alifika kwenye ofisi ya Tume ya Uchaguzi wilaya ya Kati Unguja kuomba fomu ya uteuzi.

Akiambatana na maofisa wa CCM kutoka makao Makuu, Mkoa wa Kusini Unguja, wilaya ya Kati pamoja na Jimbo la Uzini, Raza alikabidhiwa fomu hizo na masimamizi wa uchaguzi jimbo la Uzini, Mussa Ali Juma.


Akimkabidhi fomu hizo, Msimamizi huyo alimtaka mgombea huyo kuhakikisha anakijaza kila kipengele kwa umakini mkubwa na kumsisitiza ahakikishe anaisoma sheria ya uchaguzi.

Msimamizi huyo alisema Raza anatakiwa airejeshe fomu hiyo si zaidi ya Januari 24 majira ya saa 10 jioni ikiwa imedhaminiwa na wanachama kuanzia 25 waliojiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura.

Aidha Raza atatakiwa airejeshe fomu hiyo ikiwa na shilingi 200,000 za dhamana, akielezwa haki ya kukatiwa ama kukata rufaa kutoka kwa wagombea wenzake pamoja na wale sheria inaowaruhusu kufanya hivyo.

Awali kabla ya kwenda kuchukua fomu hiyo, Raza alikwenda katika ofisi za CCM wilaya ya Kati, ambapo Mwenyekiti wa CCM wilaya hiyo Hassan Shaaban alimtaka mgombea huyo hivi sasa kuwa makini.

Alisema hivi sasa ni muda wa chama kufanyakazi yake na hatapaswa kujibu ama kutoa maelezo yeyote kwani chama ndicho kitakachomsemea.

“Huu ni wakati wa tahadhari, wapo watakaokuchokoza Raza kwa kukutaka useme tu, lakini usiwajibu chama kipo kitakusemea na kujibu kila hoja”, alisema Mwenyekiti huyo.

Kwa upande wake mgombea huyo, aliwashukuru wananchi wa Uzini pamoja na wale wote waliojitokea hadi kufikia hatua hiyo.

Alisema umoja na mshikamano wa Chama ndio muhimu kwa wakati huu, na kueleza kuwa hiyo ndiyo silaha pekee itakayowasambaratisha wapinzani.

Kwa upande wao baadhi ya WanaCCM walioshindwa na Raza katika mchakato wa kura maoni wamesema kuwa makundi yao wamevunja na watamuunga mkono ili kuhakikisha jimbo hilo linarejea katika himaya ya CCM.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.