Habari za Punde

Waandishi Waisome, Waitambue Sheria ya Mtoto

Na Shifaa Said, MCT

WAANDISHI wa habari wametakiwa kuisoma na kuifahamu sheria ya No.6 ya watoto ya mwaka 2011 ili waelimishe jamii kuhusu sheria hiyo hatua ambayo itasaidia kupunguza vitendo vya ukatili na unyanyasaji dhidi
watoto.

Akizungumza hivi karibuni katika mahojiano maalum, Mwanasheria kutoka wizara ya Ustawi wa Jamii, Maendeleo ya Vijana, Wanawake na Watoto, Didas Khalfan, alisema kuwa nguvu ya vyombo vya habari haina budi kutumika katika kuelezea kwa kina sheria hiyo.


Alisema kuwa sheria hiyo ina vipengele kadhaa ambavyo kwa kiasi vitasaidia kupunguza vitendo vya udhalilishaji kwa watoto katika visiwa vya Unguja na Pemba na kueleza kuwa sheria imeweka bayana umri
wa mtoto ambaye ni yule aliye chini ya umri wa miaka 18.

Alisema kuwa katika sheria hiyo maofisa wa Ustawi wa Jamii pamoja na maofisa wa wanawake na watoto katika kila wilaya wamepewa dhamana ya kuhakikisha kuwa wanaripoti na kufuatilia kwa karibu pale wanapogundua vitendo vya ukatili kwa watoto.

Didas alikiri kuwa utafiti uliozinduliwa mwishoni mwa mwaka jana kuhusu vitendo vya ukatili dhidi ya watoto inaonyesha kuwa vitendo hivyo vipo na vinaendelea katika hatua ambayo inaathiri maisha na maendeleo ya watoto.

Utafiti huo umebainisha kuwa vitendo vya ukatili vinafanyika kwa kiasi kikubwa katika familia, majirani, skuli au vyuo hivyo alisema kuwa kuna haja ya makusudi ya jamii kushirikiana katika kufutatilia kwa karibu vitendo hivyo ili wahusika waweze kuchukuliwa hatua.

“Kuwepo kwa sheria ni kitu kimoja lakini utekelezaji wake utategemea kuwepo kwa mashirikiano baina ya familia, jamii na sehemu zote walipo watoto ili sheria hiyo iweze kutumika ipasavyo”, alisisitiza.

Alisema kuwa katika utekelezaji wa sheria ya mtoto jambo la kwanza ambalo wizara ya ustawi wa jamii maendeleo ya vijana wanawake na watoto inalisimamia ni usalama wa mtoto uwepo kwanza.

Naye mwandishi wa shirika la habari BBC, Ally Saleh alisema kuwa vyombo vya habri vinahitajika kufanya mageuzi katika kuelimisha umma athari ya vitendo vya udhalilishaji na kuibua masuala yanayowagusa watoto kwa manufaa ya jamii na taifa.

Alisema kuwa bado nguvu ya habari haijatumia ipasavyo katika kuelezea umma athari ya vitendo vya udhalilishaji hivyo nguvu hiyo haina budi kutumika ili jamii ifahamu ukubwa wa tatizo na kuweza kutoa
mashirikiano ya karibu kwa wahusika ili vitendo vya ukatili dhidi ya watoto viweze kupungua.

Alikiri kuwa wananchi wanayo matarajio makubwa ya kuwepo kwa sheria hiyo hususan kipengele cha kuanzishwa kituo cha mkono kwa mkono ambacho kitahusisha watu tofauti ambao wataweza kufuatilia kwa karibu na uharaka zaidi katika kufikia tamati ya kesi hizi za ukatili wa watoto.


Hata hivyo alikiri kuwa katika utekelezaji wa sheria hii bado kuna changamoto kadhaa ikiwemo suala zima la muhali katika kuzifiskisha kesi hizi katika vyombo vya sheria.

“Kuna haja ya kesi za udhalilishaji hususan za ubakaji kuangaliwa upya na kutizamwa kama ni suala linaloigusa serikali na jamii kwa ujumla hivyo suala la kumalizana kesi hizi katika ngazi ya polisi, au familia liwe haliwezekani”, alisema.

Naye Suzanne Kunambi mtangazaji wa shirika la utangazaji la Zanzibar akitokea redio Zanzibar alisema kuwa waandishi wa habari hawana budi kuwa karibu na jamii ili kuweza kujua jinsi gani vitendo hivi vinatendeka na pia kuibua mijadala mbali mbali mbali kupitia vyombo vya habari.

Alisema kuwa vipindi vya watoto navyo havina budi kubadilika ili watoto wenyewe wafahamu haki na wajibu wao pamoja na kufahamu kwa kina nini hasa udhalilishaji.

“Tuwashirikishe watoto katika vipindi vyetu pamoja na kuelezea kwa kina maana hasa ya udhalilishaji ili nao wafahamu hilo na wanapotendewa ukatili wowote wafahamu hatua muafaka za kuchukua”, alisisitiza.

Mkufunzi wa waandishi wa habari Suleiman Seif alisema kuwa katika mitaala ya mafunzo kwa waandishi wa habari wamejitahidi kuweka mkazo vipi waandishi wanatakiwa kuandika habari zinazowahusu watoto hususan
katika suala la udhalilishaji.

Aidha alisema kuwa Baraza la habari pia limetoa machapisho kadhaa yanaonyesha na kuelimisha kuhusua kuandika habari za watoto.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.