Habari za Punde

Dk.Shein Awa Mfano Kutaja Mali Tume

• Wanaopiga chenga waonywa

Na Kunze Mswanyama, Dar

SEKRETARIETI ya maadili ya viongozi wa umma, imesema itawachukulia hatua za kisheria pamoja na kuwafikisha kwenye baraza la maadili viongozi wa kisiasa na utumishi wa umma wanaopinga na kukaidi
kuitekeleza sheria namba 13 ya maadili ya mwaka 1995.

Katibu wa sekretarieti hiyo, Tixon Nzunda, jana aliwaeleza waandishi wa habari jijini Dar es salaam kuwa baadhi ya viongozi wamekuwa wakiikiuka sheria hiyo inayowataka kutoa maelezo ya mali zao baada ya
kukabidhiwa madaraka.


Alisema kwa mujibu wa sheria hiyo, viongozi wa kisiasa na utumishi wa umma katika kipindi cha siku 30 tangu kuteuliwa au kuchaguliwa hutakiwa kutoa maelezo ya mali zao wanazozimiliki.

Alisema kwa mujibu wa sheria hiyo, kiongozi hutakiwa kupeleka tamko la mali na madeni yake, mume au mke wake na watoto wake ambao hawajafikisha umri wa zaidi ya miaka 18, lakini viongozi hao
hawatekelezi sheria hiyo.

Alisema adhabu zilizoainishwa kwa kutoitii sheria hiyo ni pamoja na kushushwa cheo, kufukuzwa kazi, kuonywa au kushauriwa kujiuzulu au kupewa adhabu nyingine zinazoruhusiwa kwa mujibu wa sheria ama
kuchukuliwa sheria kwa mujibu wa sheria nyingine za nchi.

Katibu huyo alisema hadi kufikia Januari 13 mwaka huu, jumla ya viongozi 4,036 wa utumishi wa umma na 4,936 wa siasa walipatiwa fomu za kutolea tamko na hivyo jumla ya viongozi 8,972 walitumiwa fomu hizo.

Alisema kati ya hao 3,258 sawa na 81% ya viongozi wa siasa 4,120 sawa na 84% wa utumishi wa umma walirejesha tamko hilo ambapo ni sawa na viongozi 7,378 sawa na 82.5% ya viongozi wote.

Alisema Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, amekuwa mfano bora na wa kuigwa kwani alizirejesha fomu hizo kwa muda uliotakiwa na kuwataka wengine waige mfano huo.

Tixon, aliwataja wengine walioitii sheria hiyo ni pamoja na Rais wa Muungano, Jakaya Kikwete na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Dk. Mohammed Gharib Bilal, pamoja na wakuu wa mikoa, mawaziri, makatibu wakuu na makatibu tawala wa mikoa kwa kuwa mstari wa mbele kutii sheria hiyo.

Aidha katibu huyo alivipongeza vyombo vya habari kwa kushiriki kikamilifu kuhamasisha viongozi kuitekeleza sheria hiyo.

Tume ya maadili ya viongozi wa umma iliyoundwa kisheria kusimamia maadili ya viongozi wa umma imelenga kuwafikia viongozi wote wanaowajibika kwenye sheria hii kwani maadili mema ni mwelekeo wa kulipeleka Taifa kwenye miaka mingine 50 ya neema na mafanikio.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.