Habari za Punde

CUF Haikufanya Dhambi Kumfukuza Hamad Rashid - Maalim Seif

Chama Hakina Tabia ya kumuonea mtu

Katibu mkuu wa Chama Cha Wananchi , (CUF)ambae pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad , amesema kuwa Chama chao hakina tabia ya kumuonea Mtu wala kumpendelea bali kinafanya Shughuli zake kwa mujibu wa haki na usawa.

Ameeleza kuwa kitendo cha Baraza kuu la Chama hicho Taifa la kuwafukuza Wanachama wake hakijafanya Dhambi bali kimeteleza katiba ya Chama hicho kama ilivyoelekeza na sio kiroja kumfukuza Ubunge Hamad
Rashid Mbunge wa Jimbo la Wawi kupitia chama hicho.

Maalimu Seif, alisema hayo huko katika Kiwanja cha Gombani ya Kale wakati alipokuwa akizungumza na Wananchi na Wanachama wa Cuf , wa Mikoa miwili ya Pemba, mara baada ya kupokea maandamano ya kupongezwa kwa maamuzi ya Baraza kuu ya kuwafukuza Uwanachama wanachama wa Chama
hicho akiwemo Mbunge wa Cuf Jimbo la wawi.


Aliendelea kusema kuwa Cuf, hakijatetereka kumfukuzwa Uwanachama Mbunge wa CUF, Hamad Rashid, na wala hatorudi tena yeye na Wenzake ndani ya Chama hicho hata akienda Mahakamani.

“ Maamuzi yaliotolewa na Baraza kuu la Chama hicho , ni halali na kwamba kwa mujibu wa Katiba ya Chama hicho Wanachama hao sio wanachama tena wa CUF”alisema.

Maalim Seif, alisema kuwa Chama chake kinaheshimu Mahakama zote za Tanzania , lakini hakijapokea Barua ya Mahakama kutoka popote juu ya kusitisha kwa Mkutano huo ambao uliwavua Uwanachama wanachama wake akiwemo Mbunge wa Cuf, wa Jimbo la Wawi Hamad Rashid.

Alifahamisha kuwa Cuf, kilikuwa kinamuheshimu Mhe.Hamad Rashid kwani alikuwa muanzilishi wa Chama na Kiongozi wa Baraza kuu tokea 2002, lakini lakushangaza haijulikani Kiongozi huyo kakumbwa na masahibu gani hata akaanza kukisaliti chama hicho.

“ Cuf, haijaathirika kufukuzwa Uanachama kwa Hamad Rashid na Wenzake na kwamba hakitawarejesha tena ndani ya Chama hicho ng’o” alieleza Maalim Seif.

Alisema kuwa alipokea taarifa kutoka kwa Wabunge wa Chama hicho tokea Hamad ni Kiongozi wa Upinzani Bungeni , kuwa hawasaidii Wabunge wenzake katika Bunge, kwa vile ametingwa na majukumu makubwa na mengi na hivyo akamtaka Mwenyekiti wa Cuf, Taifa amuulize.

Maalimu , alieleza kuwa alipoulizwa na Mwenyekiti juu ya Saula hilo na kumshauri kuwa kama kazi ni nyingi apunguziwe majukumu ni yeye aliependekeza kwa kusema anawatu wawili mmoja akiwemo Mnyaa Mbunge wa Jimbo la Mkanyageni ambae alipewa nafasi hiyo kwa Uamuzi wake.

“ Cuf, haijamuonea Hamad Rashid, bali alichokipanda ndio alichokivuna Cuf, haina tabia hiyo kwani Viongozi wake wanaakili timamu wakiwemo wanasheria” alieleza.

Aliendelea kusema kuwa Chama cha CUF, hakija mfukuza Hamad Rashid , katika Bunge isipokuwa kimemfukuza Uwanachama, lakini kwa Mujibu wa sheria za Bunge huingii Bungeni mpaka uwe mbunge kutoka ndani ya Chama ama uteuliwe sasa hiyo ni kazi ya Spika atakavyoamua lakini Cuf, inaendelea kusisitiza kuwa sio mwanachama wao tena.

Nae naibu Katibu Mkuu wa Cuf, Zanzibar, Ismail Jussa Ladhu, alisema kuwa anawapongeza Wanachama wa Cuf, Kisiwani Pemba, kwa kujitokeza kwa wingi katika maandamano ya kuunga mkono maamuzi ya baraza kuu la Cuf, la kuwafukuza Uwanachama Wanachama wake waliokwenda kinyume na maadili ya chama hicho na kamwe hakitasita kwa mtu yoyote yule ataekwenda kinyume na Katiba ya chama.

Alieleza kuwa moja ya malengo ya Chama cha Cuf, ni kusimamia Wanachama pamoja na Wananchi wake lakini Hamad Rashid hata maamuzi ya kuwepo Serikali ya Umoja wa Kitaifa yeye alionekana kutoyaunga mkono.

Aliendelea kusema kuwa Cuf, imepata mitikisiko mikubwa katika kupigania Demokrasia ya Tanzania, leo itakuwa sio jambo la busara kuzarau matakwa ya Wananchi kwa kubeza lile walilolikubali kwa ridhaa yao.

Alifahamisha kuwa Cuf,haitovumilia kumuona Kiongozi wake anakwenda kinyume na Katiba ya Chama na kwamba haitamvumilia yoyote kwani itasimama kidete juu ya kusimamia maslahi ya nchi na wananchi wake kwa ujumla.

Nae Naibu Katibu Mkuu wa Cuf, Taifa, Tanzania bara, amekipongeza Chama cha CUF, kwa kuleta mabadiliko makubwa ndani ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa katika kipindi cha mwaka mmoja , kwa maana hiyo aliwataka Wananchi na wanachama wa Cuf, kuwa watulivu.

Alisema lengo la Cuf, ni kushika madaraka ya Uongozi wa Dola , hivyo waimarishe Chama chao ilikiweze kuongoza nchi katika Chaguzi zinazokuja kwani sasa hivi wamo katika Serikali lakini sio malengo makuu yao.

Wakisoma risala Wanachama wa CUF Mikoa miwili ya Pemba,iliyosomwa na Mkurugenzi waUwenezi Cuf Wilaya ya Chake Chake, Ayoub Yussuf Mgeni ,walielezakuwa wanaunga mkono maamuzi ya Baraza kuu la Cuf, kuwavua Uwanachama wanachama hao akiwemo Mbunge wa chama hicho Jimbo la Wawi Pemba.

Walisema kuwa Uwajibikaji ndani ya Chama chao ni muhimu sana kwa hivyo asie wajibika katika chama nilazima achukuliwe hatua kama hizo na kamwe Cuf, haitotetereka kwa kufukuzwa Mbunge huyo.

Risala hiyo ilieleza kuwa Hamad Alikuwa na ajenda yake ya Siri kwani alikuwa anabeza Serikali ya Umoja wa kitaifa ambayo imeleta utulivu na amani nchini kwani wamechoka kugombana lakini imeonesha dhamira yake nikutaka warejee walikotoka.

Hivyo wanakitaka Chama kutomuonea haya mtu yoyote ambae ataonekana anamwenendo mbaya na Chama hicho kwani Chama ni cha watu, na wala hakina mtu muhimu ambae hataonesha Nidhamu katika Chama 

4 comments:

  1. Bora naende Hamad Rashid. Wazanzibari tuna mengi ya kuyashughulikia wakati huu. Hatustahiki wala wahustahmili usaliti.

    ReplyDelete
  2. Hamadi Rashid na Shamhuna wako kundi moja naomba CCM Zanzibar mshughulikieni Shamhuna, nchi anaiuza kwa kutegemea urais 2020.

    ReplyDelete
  3. Haya ndiyo matatizo ya kua na jamii yenye uwezo wa kufikiri namna moja tuu!..kila unae muona'maalim..keshasema!..maalim keshasema!

    Watu wakumbuke huyo maalim nae ni binadamu ana mapungufu yake.
    Kwa kweli haiingii akilini, kwamba Hamad Rashid aisalini CUF sasa hivi, wakati alikua na mazingira mazuri zaidi miaka 20 iliyopita.

    Pili watu wanadanganya wenzao kwamba Hamad anashirikiana na CCM bara ili kuiua CUF kwa vile hiki ni chama tishio.

    Ukweli ni kwamba CUF kwa sasa si chama tishio tena kwa CCM bali chama tishio ni CHADEMA. CCM wanaihitaji zaidi CUF ili washirikiane kupambana na CHADEMA.

    Wanaoeneza uvumi wa namna hiyo juu ya Hamd rashid wana 'take advantage' ya Wza'bari wengi kutokua na uwezo wa kuhoji mambo na kufukiri pande mbili.

    Ama mimi nasema siku zote, kwa mazingira ya chama kama CUF,.. hata mimi mbumbumbu naweza kua kiongozi..tena mzuri tuu!!!

    ReplyDelete
  4. Kwa mtu mwenye kufuatilia siasa za hapa kwetu, hawezi kusema kua SHAMHUNA anaiuza nchi kwa kutarajia urais wa 2020.

    SHAMHUNA ni mmoja wa WAZANZIBARI amba nchi inawauma na ni kutokana na msimamo huo ndio maana yeye ktk CCM ni mwanachama tuu, vyeo vingine vyote ..amepokwa.

    Ana matatizo yake mengine tuu..lakini sio hayo
    ...fatilieni mambo jamani..mtauzwa!!!ndani ya nchi yenu wenyewe.

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.