Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mheshimiwa Said Ali Mbarouk akitoa maelezo mafupi kuhusiana na ujenzi wa jengo jipya la makao makuu ya Wizara hiyo lililoko Maruhubi katika hafla ya ufunguzi uliofanywa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akifunua pazia kuashiria ufunguzi rasmi wa jengo jipya la Makao Makuu ya Wizara ya Uvuvi na Mifugo huko Maruhubi mjini Zanzibar. Nyumani kwake ni Waziri wa Wizara hiyo Mheshimiwa Said Ali Mbarouk
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza katika hafla ya ufunguzi wa jengo jipya la Makao Makuu ya Wizara ya Uvuvi na Mifugo huko Maruhubi mjini Zanzibar. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Mheshimiwa Abdallah Mwinyi Khamis.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amesema utekelezaji wa sheria za uvuvi hauna lengo la kuwakomoa wavuvi na wananchi bali ni kuleta ustawi kwa jamii na taifa kwa jumla.
Maalim Seif ametoa kauli hiyo alipokuwa akifungua jengo la Makao Makuu ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi huko Maruhubi mjini Zanzibar ikiwa ni katika shamra shamra za maadhimisho ya miaka 48 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Amesema wakati serikali ikiandaa mipango yake ya maendeleo katika sekta ya uvuvi, wananchi hawanabudi kuunga mkono mipango hiyo kwa kufuata sheria zilizowekwa na wasione vibaya au kuhisi wameonewa wakati serikali inaposimamia sheria hizo.
Ameitaka wizara ya mifugo na uvuvi kuwaelimisha wavuvi juu ya umuhimu wa kufuata sheria hasa katika maeneo ya hifadhi ya bahari na kuondokana na dhana kuwa serikali inawaonea.
Amefahamisha kuwa lengo la serikali ni kuwawezesha wananchi na kwamba juhudi za kuanzisha benki ya mikopo kwa ajili ya wakulima, wavuvi, wafugaji na wajasiriamali wengine iko mbioni, ikiwa na lengo la kuwawezesha wananchi kujikwamua na umaskini.
“Si muda mrefu tunataka kiwepo chombo cha aina hiyo ili tuweze kuwasaidia wazanzibari”, alidokeza Maalim Seif.
Maalim Seif amesema kuwa mkazo wa serikali kwenye sekta ya uvuvi na mifugo ni kuzitanua sekta hizo ili ziweze kuleta tija kwao ikiwa ni pamoja na kuongeza nafasi za ajira, ikizingatiwa kuwa sekta hizo zinawahusisha watu wengi zaidi.
Makamu wa Kwanza wa Rais ametumia fursa hiyo hiyo kuwaasa wavuvi kufanya shughuli zao bila kuleta athari za kimazingira ya bahari.
Kwa Upande wake Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mheshimiwa Said Ali Mbarouk amesema Wizara hiyo inakusudia kufanya Mapinduzi ya uvuvi na mifugo kwa kuwawezesha wavuvi kuvua katika bahari kuu na kuepukana na uvuvi haramu.
“tunakusudia kuufanya mwaka huu wa 2012 kuwa mwaka wa mapinduzi katika sekta zetu hizi na utakuwa mwaka wa kutokomeza uvuvi haramu” alisema Mhe. Mbarouk.
Ameongeza kuwa Wizara hiyo inashirikiana kwa karibu na Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko kuitafutia ufumbuzi bei ya mwani duniani ili iendane na mahitaji ya wakulima na gharama za uendelezaji, na kwamba kuna matumaini ya mafanikio.
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bwana Kassim Gharib Juma amesema Wizara inajipanga ili kuifanya sekta ya uvuvi iwe na tija zaidi kwa wavuvi ikiwa ni pamoja na kuharakisha mipango ya kuwawezesha kuvua katika bahari kuu.
Ujenzi wa jengo hilo lijuikanalo kwa jina la “Nyangumi House” umegharimu dola za kimarekani milioni mbini na nusu na umetekelezwa na mradi wa MACEMP chini ya ufadhili wa mkopo kutoka Benki ya Dunia WB.
Hassan Hamad (OMKR).
Naipongeza sana, SMZ kwa juhudi zeke za kuiletea Z'bar maendeleo. Naamini walio wengi watajiuliza hapo katikati palitokea nini mpaka maendeleo yakadorora.
ReplyDeleteUjenzi wa majengo ya namna hii ni muhimu kwa vile yanaupa nafasi Mji mkongwe kubaki kama mji wa kitalii kwa kuupunguzia harakati za kiutawala.
Hata hivyo, athari za ule wimbo wangu wa kawaida wa kuiomba SMZ kutenga maeneo maalum (prime areas) kwa ajili ya majengo ya serikali pamoja na viongozi bado inajitokeza.
Leo hii majengo mengine ya serikali yapo Maruhubi, mengine migombani, mengine mazizini, mengine maisara. Sisemi kuna ubaya katika hilo lakini yakiwa pamoja inapendeza kiustawi na kiulinzi.
Watu wanapiga kelele kwamba ofisi zote za kibalozi za TZA ziko Dar, lakini wanasahau kwamba SMT ikiamua kuhamishia Z'bar baadhi yake leo hii Z'bar itabidi wapelekwe Tunguu, wakati DAR wametengewa maeneo 'nyeti'