Habari za Punde

Mazishi ya Sumari Yageuzwa Ulingo wa Kisiasa

Na Joseph Ngilisho, Arusha

MSIBA wa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki juzi uligeuzwa kuwa ulingo wa kisiasa, baada ya kundi la vijana wafuasi wa chama kimojawapo cha siasa nchini kuibuka na kupiga makelele ya ‘people
power’.

Kama hiyo haitoshi vijana hao walimuonesha vidole viwili Rais Jakaya Kikwetwe, aliyehudhuria mazishi hayo wakati akielekea nyumbani kwa marehemu kwa ajili ya mazishi.


Fujo lililfanywa na vijana hao, liliwafanya baadhi ya viongozi wakiwemo mawaziri kushindwa kula chakula kutokana na vumbi walilokuwa wakirusha.

Kundi hilo lilionekana kujipanga makusudi kwa ajili ya kuvuruga mazishi hayo, kwani walikuwa wakihamasisha watu kwa kuinua vidole viwili juu, huku Mbunge wa Arusha mjini Godbless Lema akiwaunga mkono, hali iliyosababisha msiba huo kugeuka uwanja wa siasa na watu kusahau kwamba wapo msibani.

Hatua ya fujo hizo walizokuwa wakifanyiwa viongozi wa serikali waliohudhuria mazishi hayo ziliwakera baadhi ya makada wa Chama cha Mapinduzi, wakiwemo vijana wa Green Guard.

Vijana hao wa CCM walimuondosha kwa nguvu Mbunge huyo aliyekuwa akishabikia vurugu za vijana hao na baadae kuwasaka wale wote waliosababisha vurugu hizo.

Kutokana na hali hiyo hali ya hewa kuchafuka ghafla eneo la msiba na kutawaliwa na vumbi, ambapo viongozi mbalimbali wakiwemo wa serikali na wageni mbali mbali, walichafuka vumbi mithili ya mtu aliyekuwa akichimba shimo.

Ingawa hali hiyo haikuleta madhara makubwa, baadhi ya watu walisikika wakilalamikia jeshi la Polisi kushindwa kudhibiti hali hiyo kwa kuwakamata vijana hao waliokuwa wakileta fujo.

Vituko hivyo vimelalamikiwa sana na wananchi waliohudhuria mazishi hayo wakidai kwamba hatua ya kuanza kampeni sehemu ya msiba haikuwa sahihi, bali wahusika wameonesha kitendo kisicho cha kistaarabu.

Wakati hayo yakiendelea waziri mkuu Mizengo Pinda pamoja na baadhi ya mawaziri wake walikuwa bado hawajaondoka eneo hilo la mazishi kwani baadhi yao walishuhudia vurugu hizo na kukumbwa na adha ya kuchafuka na vumbi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.