Habari za Punde

Serikali Itaendelea Kuwaunga Mkono Wasanii wa Uchoraji

Na Rajab Mkasaba

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar itaendelea kuwaunga mkono wasanii wa fani ya uchoraji wakiwemo vijana kwani hatua hiyo itachangia kuwawekea mazingira mazuri ya kujiajiri pamoja na kuimarisha sekta ya utalii nchini.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein aliyasema hayo leo Ikulu mjini Zanzibar baada ya kukabidhiwa picha iliyochorwa kwa penseli na mchoraji Haji Simba kutoka kikundi cha ZAN Artists chenye maskani yake Hurumzi mjini Zanzibar inayoonesha akichuma karafuu.


Akitoa pongezi zake kwa kijana huyo pamoja na kamati maalum iliyoratibu usanii huo, Dk. Shein alisema kuwa sanaa ya uchoraji ina nafasi kubwa katika kuendeleza ajira hasa kwa vijana na kuimarisha sekta ya utalii hapa Zanzibar.

Alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kutambua thamani na umuhimu wa sanaa ya uchoraji imeamua kwa makusudi kuwatafuta wale wasanii wote wa zamani wa fani hiyo ili wawaweke pamoja kwa lengo la kukimarisha sanaa hiyo.

Dk. Shein alieleza kuwa wasanii hao wakongwe wataweza kusaidiana kwa karibu na vijana hao wanaochipukia katika fani ya uchoraji na kuweza kusukuma mbele juhudi hizo za serikali.

Aidha, Dk. Shein alikubali kuwa mlezi wa kikundi hicho ambacho kinatarajia kuanzisha SACCOS itakayowakusanya pamoja vijana hao ambapo kwa kuanzia amewaahidi kuwapa shilingi milioni tatu kwa ajili ya kujiimarisha zaidi.

Dk. Shein aliisifu na kuiponmgeza kazi hiyo iliyofanywa na Simba na kueleza kuwa jitihada zake zimemtia moyo sana na kusisitiza azma ya kuwawezesha ili kwa kila mmoja aweze kujiajiri mwenyewe. “Vitu kama hivi vina umuhimu mkubwa na iwapo tukiwasaidia vijana wetu, watafanikiwa na tutatunza historia yetu vizuri ’,alisema Dk. Shein.

Aidha, alieleza kuwa hatua hiyo itaimarisha sekta ya utalii ambayo kwa hivi sasa imekuwa ikichangia kwa kiasi kikubwa pato la taifa na ndio maana akawa anatilia mkazo kauli mbiu ya utalii isemayo ‘Utalii kwa Wote’ ili kila mwananchi ajue kuwa anawajibu wa kuutangaza utaalii kwa njia nzuri.

Dk. Shein pia, alitoa pongezi kwa Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) kwa kuidhamini picha hiyo pamoja na wadau mbali walioshiriki ukiwemo uongozi wa Kamisheni ya Utalii, Jumuiya ya ZATI, Idara ya Utamaduni, wapiga picha na waandishi wa habari na kusisitiza haja ya kutangwazwa zaidi kwa sanaa hiyo.

Mapema Mshauri wa Rais Utalii Bwana Issa Ahmed, alimueleza Dk. Shein kuwa hatua hiyo ni miongoni mwa juhudi zinazochukuliwa katika kuinua sekta ya utalii sanjari na kuwajengea uwezo vijana ili waweae kujiajiri wenyewe.

Alisema kuwa picha hiyo yenye kuonesha Dk. Shein akichuma karafuu ni alama muhimu inayoonesha ni kwa jinsi gani Dk. Shein ameshiriki katika kuliimarisha na kulitunza zao la karafuu ambalo linachangia pato la taifa.

Nae Mratibu wa shughuli hizo Simai Mohamed alimueleza Dk. Shein kuwa tukio la Rais Dk. Shein kuchuma karafuu ndio chachu ya kazi hiyo.

Alieleza kuwa picha hiyo imechorwa kwa kutumia penseli na ina uwezo wa kudumu kwa muda wa miaka 100, ilichorwa kwa muda wa siku 60 ambapo ilianza Septemba 20 hadi kumalizika Novemba 20.

Alisema kuwa picha waliyomkabidhi Dk. Shein ni mchango wa wasanii baada ya kuguswa na juhudi zake anazozichukua katika kuimarisha zao la karafuu ambalo linamchango mkubwa katika ustawi wa wananchi wa Zanzibar.

Nae mchoraji wa picha hiyo Haji Simba, alieleza kufarajika kwake kutokana na Rais kuikubali na kuipokea kwa furaha kubwa picha hiyo na kueleza jinsi alivyoichora picha hiyo kwa umakini na umahiri zaidi kwa vile ni picha ya kiongozi huku akimuomba Rais kuwa mlezi wa kikundi chao.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.