Na Salum Vuai, Maelezo
Mabingwa watetezi wa Kombe la Mapinduzi, Simba, wameonja kipigo katika mchezo wa kwanza mbele ya Jamhuri kutoka Pemba, kwa kuchapwa mabao 2-1 juzi usiku katika uwanja wa Amaan.
Timu zote ziliuanza mchezo kwa kasi huku zikishambuliana kwa zamu, ambapo Simba ilitawala sehemu ya kiungo iliyokuwa na Jamal Mkude, na Edward Christopher, nayo Jamhuri ikicheza vyema sehemu ya ulinzi
kuwazuia washambuliaji matata wa Simba kina Felix Sunzu na Gervas Kago.
Hata hivyo, miamba hiyo ilikwenda mapumzikoni bila kuzifumania nyavu, na kuanza kipindi cha pili zikiongeza kasi na kutoa burudani kwa mashabiki wengi waliojazana uwanjani hapo.
Mnamo dakika ya 55, akiwa ndio kwanza ameingia kuchukua nafasi ya Victor Costa, mchezaji Kevin Yondani alishindwa kuudhibiti mpira na kumruhusu Ali Othman amzunguke kabla kumvisha kanzu mlinda mlango Ali Mustafa aliyekuwa ametoka golini na kuiandikia Jamhuri bao la kwanza.
Nyavu za Simba zilichanwa tena katika dakika ya 65, kwa bao la Bakari Khamis alipoubetua juu mpira na kufunga kwa kichwa, baada ya mlinzi wa Simba Juma Nyoso kucheza na mpira bila tahadhari.
Jitihada na presha za Simba langoni mwa Jamhuri, ziliipatia bao katika dakika ya 74 lililofungwa na Shomari Kapombe, kufuatia piga nikupige iliyotokana na mpira wa kona iliyochongwa na Ramadhani Singano.
Wakati huohuo, kamati ya mashindano hayo imesema pambano hilo liliingiza shilingi 8,280,000, na lile la mchana kati ya KMKM na Miembeni United, kuambulia shilingi 220,000.
No comments:
Post a Comment