Habari za Punde

Tibaijuka Atinga Ofisi za UN

Alifikisha ombi kudai nyongeza eneo la bahari

Mwandishi maalum, New York

JAMHURI ya Muungano wa Tanzania, imewasilisha katika Umoja wa Mataifa, Andiko la kudai eneo la nyongeza lenye ukubwa wa maili 16,000 nje ya eneo la sasa la maili 200 za ukanda wa kiuchumi wa bahari.

Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Anna Tibaijuka, ndiye aliyewasilisha andiko hilo, kwa niaba ya serikali, katika hafla fupi iliyofanyika juzi katika ofisi za Idara ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia masuala ya bahari na sheria ya bahari.


Andiko hilo limepokelewa na Mkurugenzi wa Idara hiyo, Sergei Tarassenko kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, ambaye aliipongeza Tanzania kwa hatua hiyo muhimu na kuahidi kwamba Idara yake kupitia, Kamisheni ya Umoja wa Mataifa inayohusika na mipaka ya baharí italifanyika kazi andiko hili.

Aidha Mkurugenzi huyo aliielezea Tanzania, kama moja kati ya nchi inayoheshima sana na yenye historia nzuri katika Umoja wa Mataifa.

Akizungumza wakati wa kuwasilisha andiko hilo, waziri Anna Tibaijuka, alisema kwa kuwasilisha andiko hilo, Tanzania si tu kwamba imefanya kazi ya uhakika ya maandalizi na hatimaye uwasilishaji lakini ni hatua kubwa kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Akabanisha kwamba mchakato wa maandalizi ya andiko hilo ambao umechukua miaka mitano, umewashirikisha wataalamu mbalimbali wakiwamo wa ndani na nje, ikiwa ni pamoja na kuzihusisha nchi ambazo zinapakana kibahari na Tanzania.

“Tanzania itanufaika kwa kuongeza ukubwa wa eneo la mipaka ya nchi lakini la msingi zaidi ni unufaikaji wa rasilimali zikiwamo za mafuta na gesi na madini ambazo zitakuwamo katika eneo hilo jipya, rasilimali ambazo kwa sasa zinaelekea kutoweka katika eneo la maili 200”, alisema Tibaijuka.

Eneo ambalo Tanzania inadai liongezwe la maili 61, 000 ukubwa wake ni sawa na eneo la mikoa mitatu ikiunganishwa kwa pamoja.

Aidha kuongezwa kwa eneo hilo kutaisaidia pia serikali katika masuala ya ulinzi na usalama hasa katika kipindi hiki ambacho vitendo vya uharamia wa baharini vikiwa vimeongeza katika eneo la bahari ya Hindi.

Baada ya kuwasilisha andiko hilo, hatua inayofuatia ni kwa Tanzania kupitia wataalamu wake, itatakiwa kulitetea andiko hilo mbele ya Makamishna wa Kamisheni ya Umoja wa Mataifa inayohusika na mipaka ya bahari utetezi huo utafanyika mwezi Agosti mwaka huu.

Tanzania imewasilisha andiko hilo kwa kuzingatia sheria ya kimataifa ya bahari namba 76 kifungu kidogo cha 4, sheria hiyo inaziruhusu nchi ambazo ziko kando kando ya bahari kudai eneo la nyongeza iwapo zitakidhi vigezo vilivyotolewa na Umoja wa Mataifa.

Mchakato wa kuanda Andiko hilo ulianza mwaka 2007 ukiwashirikisha wataalamu wa kada mbalimbali kutoka Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Chuo Kikuu cha Ardhi na Mazingira, Wizara ya Sayansi na Teknolojia na Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC).

Hafla ya kuwasilisha andiko hilo imehudhuriwa na Balozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Ombeni Sefue, na waheshimiwa wabunge, Zakhia Meghji na Abulrahman Hassan Shah ambao ni wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira.

Wengine waliohudhuri hafla hiyo ni baadhi ya wataalamu waliohusika na maandalizi ya Andiko hilo ambao ni Dk. Sellasie Mayunga, Prof. Evelyne Mbende, Ayoub Mohamed Mahmoud kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Kelvin Komba na Verdiana Mashingia.

Tanzania inakuwa nchi ya 59 kuwasilisha andiko la kudai nyongeza ya eneo la bahari na ikiwa ni nchi 10 kutoka Afrika kufanya hivyo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.