Yunus Sose,ZBC
WAZIRI wa Habari, utamaduni, Utalii na Michezo Abdilah Jihad Hassan amevihimiza vyombo vya habari na vikundi vya sanaa nchini kuongeza kasi ya kuelimisha ili kuzuia kuporomoka kwa maadili ya Mzanzibari.
Alisema vyombo vya habari vinaweza kutoa mchango katika kuirejeshea hadhi yake Zanzibar ambayo inazidi kutishiwa na mila za kigeni zinazoingizwa nchini kwa njia mbali mbali.
Waziri wa Habari alisema lazima kuandaliwe mikakati itakayosimamiwa na vyombo vya habari kwa kuwa Zanzibar ina historia yake inayoweza kupotezwa endapo vikundi vya sanaa na vyombo vya habari havitasimama imara kuulinda ytamaduni wa nchi.
Waziri Jihad ametoa msimamo huo wakati akifungua semina ya siku moja ya kuweka mikakati ya pamoja ya kuzuia kuporomoka maadili na kuirejeshea Zanzibar hadhi yake iliyogubikwa na tamaduni za kigeni.
Semina hiyo, maalum kwa masheha, viongozi wa vikundi vya sanaa, Makamanda wa Polisi wa Mikoa, Viongozi wa dini pamoja na vyombo vya habari, ilifanyika ukumbi wa hoteli ya Bwawani.
Alisema jamii haiwezi kukwepa ukweli kuwa vyombo vya habari vimechangia uporomokaji maadili lakini akatoa changamoto kwa kusema vyombo hivyo hivyo, vibebe fursa nyengine kuiongoza jamii kurejesha
maadili mema yenye matumaini kwa wananchi.
"Katika suala la kuporomoka kwa maadili hakuna wa kuonyooshewa kidole moja kwa moja lakini kazi iliyobakia ni kushirikiana pamoja katika kupambana na changamoto zinazoikabili jamii na bila shaka
tutafanikiwa," alisema Jihad.
Waziri Jihad alisema ni vipi wanajamii wanaweza kukwepa wajibu wao ili kuiacha nchi na hasa vizazi vya kesho kukosa mwelekeo kwa sababu utamaduni wa asili umeshavurugwa.
Akiwasilisha mada inayohusiana na majukumu ya bodi ya sensa, filamu na sanaa za maonyesho Zanzibar, Katibu Mtendaji wa Bodi ya Sensa na Filam za maonyesho Suleiman Mbarouk Suleiman, alisema kutokana na uwezo mdogo wa bodi kifedha bodi hiyo inashindwa kutekeleza kwa ufanisi majukumu yake likiwemo la kufikisha elimu ya kutosha kwa wananchi wengi vijijini.
Semina hiyo ilifungwa na Katibu Mtendaji wa BAKIZA na Kaimu Kamishna wa Utamaduni na Michezo Zanzibar,Khadija Bakari Khatib.
No comments:
Post a Comment