Na Abdi Shamnah
WAZIRI wa Habari,Utamaduni,Utalii na Michezo, Jihad Hassan amewataka wasanii nchini nchini kujenga umoja na mshikamano ili kukabiliana na wimbi la wizi wa kazi zao.
Amesema bila ya kuwepo chombo cha kuwaunganisha pamoja, daima thamani ya kazi zao itapotelea katika mikono wa wajanja wachache.
Jihad ametoa changamoto hiyo jana katika ukumbi wa Tume ya Utangazaji, Kikwajuni, wakati alipokutana na kubadilishana mawazo na wasanii wa filamu na maigizo kutoka Bara na Zanzibar, baada ya kukamilika kwa Tamasha la ZIFF.
Alisema kuna umuhimu mkubwa kwa wasanii hao kufanya kazi kwa mashirikiano ya karibu, na kuwaomba magwiji wa sanaa kutoka Bara kuwasidia wenzao wa Zanzibar, ambao kiwango chao cha uigizaji kipo chini.
Aliwataka wasanii hao kutilia maanani uendelezaji wa mila, desturi na maadili ya Watanzania, katika filamu zao.
Aidha aliwataka kuelekeza nguvu zao katika kuigiza filamu zinazonyesha uhalisia wa maisha ya Mtanzania, badala ya kuegemea maisha ya kifahari.
‘Kuna filamu nyingi zilizoegemea katika maisha ya kifahari, ni vyema kuelekeza nguvu zenu katika filamu zinazendana na maisha halisi ya Watanzania, ambapo wengi wao ni masikini’, alisema.
Waziri Jihad alisema Serikali zote mbili zinalenga kuinua viwango na kulinda kazi za wasanii na kuainisha kuwa Wizara yake imo mbioni kujenga Studio ya kisasa ya kurekodia.
No comments:
Post a Comment