Habari za Punde

Hisa za Zanzibar BoT Zaendelea Kujadiliwa

SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) wanaendelea na mazungumzo kuhusu suala la hisa ya asilimia 11.5 ya Zanzibar ndani ya Benki Kuu (BoT).

Fedha hizo zinadaiwa kuhamishwa katika benki hiyo baada ya kuvunjika kwa Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki. Naibu Waziri wa Fedha, Pereira Ame Silima amesema kwamba suala hilo halipo wazi na linafanyiwa mazungumzo na kutaka wabunge na wananchi wa Zanzibar kuvuta subira.


Kauli hiyo ya Naibu Waziri ililenga kujibu swali la nyongeza la Mbunge wa Magogoni, Hamad Ali Hamad (CUF) ambaye alitaka kufahamu hisa za Zanzibar kwenye benki hiyo ambazo katika swali la msingi halikuelezwa.

Katika swali la msingi, Mbunge wa Kojani, Rashid Ali Omar (CUF) alitaka kufahamu kama Tanzania Zanzibar imeshawahi kupata hisa zake kupitia BoT kwa kuwa kuna taarifa kwamba SMZ ni mteja wa mwanzo wa benki hiyo.

Naibu Waziri alisema katika jibu lake la msingi kwamba Benki Kuu iliyoanzishwa mwaka 1965 chini ya Sheria ya Bunge ni chombo kinachomilikiwa na Jamhuri ya Muungano. Alisema chini ya sheria hiyo, hisa zote zinamilikiwa na Jamhuri ya Muungano ambayo inaundwa na Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar.

Aidha, alisema hali hiyo imeainishwa pia katika sheria ya sasa ya Benki Kuu ya mwaka 2006. Pia Naibu Waziri alisema mtaji ulioanzisha BoT ilipoanza shughuli zake mwaka 1966, ulitolewa na Hazina ya Jamhuri ya Muungano na mwenye dhamana ya hisa hizo kama ilivyo kwa mashirika yote ya umma ni Msajili wa Hazina.

Pia alisema kwamba Kifungu cha 14(2) cha sheria hiyo iliyoanzisha Benki Kuu kinaeleza wazi kwamba ni Jamhuri ya Muungano pekee ndiyo inaweza kisheria kumiliki hisa (mtaji) za BoT.

Chanzo: Habari Leo

1 comment:

  1. Watanganyika wanajulikana dunia nzima kama ni wezi na wadanganyifu na wenye roho dhaifu,hakuna cha mazungunzo.Solution vunya muungano au serekali tatu.
    Mungu ibariki zanzibar

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.