Habari za Punde

Ufaulu Kidato cha Nne Waongezeka Asilimia 2.63

 Waliojibu matusi wafutiwa matokeo

Na Mwandishi Wetu

WATAHINIWA 225,126 sawa na asilimia 53.37 wamefaulu mtihani wa kidato cha nne iliyofanywa mwaka 2011, ikiwa ni ongezeko la asilimia 2.63 la ufaulu ikilinganishwa na mwaka mwaka 2010 uliofaulisha wanafunzi 223,085.

Akitoa matokeo ya mtihani wa kitado cha nne jana jijini Dar es Salaam, Katibu wa Baraza la Mitihani Tanzania, Dk. Joyce Ndalichako alisema ubora wa ufaulu kwa watahiniwa wa skuli umeonesha kuwa jumla ya watahaniwa 33,577 sawa na asilimia 9.98 wamefaulu katika madaraja ya I hadi la III.


Alisema wasichana waliofaulu katika madaraja I hadi la III ni 10,313 ambao ni sawa na asilimia 7.13 na wavulana 23,264 sawa na asilimia 12.13.

Dk. Ndalichako aliwataja watahiniwa 10 bora kitaifa katika mtihani huo ni pamoja na Moses Andrew Swai kutoka Feza (Dar es Salaam), Rosalyn A Tandau Marian Girls (Pwani), Mboni Maumba St. Francis Girls (Mbeya), Sepiso Mwamelo St. Francis (Mbeya) na Uwella Rugaba Marian Girls (Pwani).

Wengine ni Hellen S. Mpanduji St. Mary Mazinde Juu Tanga, Daniel Wallance Maugo St. Joseph Dar es Salaam, Benjamin J.Tilubuzya Thomas More Machrina Dar es Salaam, Simona William Mbangalukela St. Joseph Millennium Dar es Salaam na Nimrod Deocles Rutatora Feza Boys Dar es Salaam.

Wasichana 10 bora katika mitihani hiyo ni Rosalyn A. Tandau Marian Girls (Pwani), Mboni Maumba St. Francis Girls (Mbeya), Sepiso Mwamelo St. Francis (Mbeya), Uwella Rugaba Marian Girls (Pwani) na Hellen S. Mpanduji St. Mary Mazinde Juu (Tanga).

Wengine ni Lisa Chille St. Francis (Mbeya), Elizabeth Ng’imba St. Francis (Mbeya), Doris Atieno Noah Kandoto Sayansi Girls (Kilimanjaro), Herieth Machunda St. Francis Girls (Mbeya) na Daisy Mugenyi Kifungilo Girls (Tanga).

Kwa upande wa wavulana 10 bora kwenye mitihani hiyo ni Moses Andrew Swai Feza Boys (Dar es Salaam), Daniel Wallace Maugo St. Joseph Millennium (Dar es Salaam), Benjamin J. Tilubuzya Thomas More Machrina (Dar es Salaam), Simon William Mbangalukela St. Joseph Millennium (Dar es Salaam) na Nimrod Deocles Rutadora Feza Boys (Dar es Salaam).

Wengine ni Simon Gabriel Mnyele Feza Boys (Dar es Salaam), Paschal John Madukwa Nyegezi Seminari (Mwanza), Henry Justo Stanley Mzumbe (Morogoro) na Tumain Charles Ilboru (Arusha).

Katibu huyo alizitaja skuli 10 bora zilizokuwa na watahiniwa 40 na zaidi ni pamoja na St Francis ya Mbeya, Feza Boys Dar es Salaam, St. Joseph Millennium Dar es Salaam, Marian Girls Pwani na Don Bosco seminary Iringa.

Nyengine ni Kasita seminary Morogoro, St. Mary Mazinde Juu Tanga, Canossa Dar es Salaam, Mzumbe Morogoro na Kibaha Pwani.

Dk. Ndalichako alisema kwa mujibu wa kifungu 52(b) cha kanuni za mitihani matokeo ya watahiniwa 3,303 walibainika kufanya udanyanifu wa aina mbali mbali kwenye mitihani hiyo.

Miongoni mwa udanyanyifu waliobainika kuufanya ni pamoja na kukamatwa katika vyumba vya mitihani wakiwa na ‘notes’, kukamatwa na simu ndani ya vyumba vya mitihani, kufanyiwa mitihani na watu wengine, kubainika kufanya mitihani kwa majina ya watu wengine ambao wameshafanya mitihani hiyo.

Makosa mengine ni kubainika kuwa na mfanano wa majibu usio wa kawaida, kubainika kuwa script zenye maandiko, watahiniwa kubadilishana karatasi za masuali/vijitabu vya kujibia mitihani.

Aidha alisema Baraza la Mitihani Tanzania limefuta matokeo ya watahiniwa wanane walioandika matusi katika script, kitendo ambacho ni kosa kwa mujibu wa kifungu 5(13) cha kanuni za mitihani.

Alisema kitendo cha kuandika matusi kwenye karatasi za majibu kinaonesha utovu wa nidhamu ambapo baraza hilo halitaweza kuwavumilia watahiniwa hao hivyo watafuatiliwa ili kuchukulia hatua zaidi.

“Tahiniwa wote waliofutiwa matokeo yao kutokana na udanganyifu au kuandika matusi kwenye karatasi za majibu hawataruhusiwa kufanya mitihani ya Baraza kwa kipindi kisichopungua miaka mitatu”,alisema Ndalichako.

Katika mitihani hiyo jumla ya vituo 4,795 vilitumika kufanyia mitihani hiyo, ambapo wanafunzi 450,324 walisajiliwa kufanya mitihani hiyo ambapo wasichana ni 201,799 na wavulana 248,525.

1 comment:

  1. Pamoja na kuongezeka kwa kiwango cha ufaulu kitaifa, mimi bado nalia na nyumbani Z'BAR

    Kwetu bado kuna matatizo makubwa ktk kusimamia mfumo wa elimu, pamoja na kuwa na wataalam wengi wa fani hiyo.

    Mimi nna wasi wasi sana na namna wizara inavyofanya 'evaluation' ya watoto wa FORM 11
    yaani namna mitihani inavyo tungwa, kusahihishwa,pamoja na uteuzi wa wale wanaofaulu.

    Hivi inakuwaje wanafunzi wanaofaulu kwa maelfu wakiwa FORM 11 baadae karibia asilimia 70 washindwe kuendelea na masomo ya juu?

    Baada ya kufeli watu wanatoa tuhuma za 'kijinga'
    eti tunaonewa na kua tunafelishwa makusudi!

    Hata wale ambao hufanikiwa kuendelea na masomo hayo, na wizara kujisifia, huishia kusoma masomo ya KISWAHILI, DINI na KIARABU.

    Baada ya hapo, watoto hao huelekea CHUO CHA KIISLAMU na kuishia Chukwani kwa ajili ya DEGREE za masomo ya dini.

    Wakati wote huo kitengo cha MIPANGO CHA WIZARA YA ELIMU kinaona,.. hatimae WIZARA inakuja kusema kua hawahitaji walimu wa namna hiyo na hivyo hawatowaajiri..huku wameshawapotezea muda.

    Jamani tukumbukeni hakuna nchi iliyowali kupiga hatua duniani kwa kuchezea mfumo wake wa elimu.

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.