Na Mwantanga Ame
SERIKALI ya China inakusudia kuipatia miradi minne itayoweza kuinufaisha Serikali ya Zanzibar na wananchi ikiwa ni hatua ya kuongeza ushirikiano kati ya nchi mbili hizi.
Balozi mdogo wa China aliyepo Zanzibar, Chen Qiman, aliyasema hayo jana wakati akizungumza na Waandishi wa Habari, baada ya kupokea taarifa ya Watendaji Wakuu wa Serikali ya Zanzibar, waliofanya ziara ya kimafunzo nchini China.
Alisema serikali ya China inakusudia kutoa msaada huo ambapo wiki ijayo itasaini mikataba minne na serikali ya Zanzibar, ukiwemo wa kujenga Hospitali mpya ya Mkoani kisiwani Pemba ambayo itakuwa na vifaa vya kisasa.
Mkataba mwengine ambao aliutaja kusainiwa ni ujenzi Jengo jipya la Wagonjwa Mahatuti ICU, katika Hospitali ya Mnazimmoja na Mradi wa Usambazaji wa taa zinazotumia nishati ya jua katika Mji wa Zanzibar.
Alisema Mradi mwengine ambao utausaini utahusu ujenzi wa skuli ya kisasa ya msingi katika eneo la Mwanakwerekwe pamoja na kukamilisha mradi wa Mkonga wa Taifa ‘E-government’ itaukabidhi rasmi mwezi Aprili mwaka huu.
Hata hivyo, balozi huyo pia alisema suala jengine ambalo serikali hiyo italizingatia ni kuwapatia mafunzo zaidi wananchi wa Zanzibar katika suala la uvuvi ambapo itawafunza wanawake na wanaume.
Balozi huyo alisema amefurahishwa na hatua ya watendaji wa serikali ya Zanzibar kukubali kuthamini mafunzo hayo kwani yataweza kuisaidia serikali kuwa na mabadiliko katika uchumi wake.
Alisema serikali ya China hivi sasa imeweza kupiga hatua mbali mbali za kimaendeleo lakini Wazanzibari wanapaswa kutambua hayakuweza kuja kwa haraka bali wananchi wa taifa hilo waliamua kujituma zaidi.
Alisema China, hivi sasa imekuwa ni ya pili duniani uchumi wake baada ya kufanikiwa kuyafikia vyema masoko ya dunia likiwemo WTO huku ikiamua kuachana na sera za zamani ya uchumi kwa ajili yao.
Alisema kufunguka kwa masoko hayo hivi sasa serikali hiyo imeweza kuyatumia vyema maneo ya ukanda wa biashara huru jambo ambalo limewafanya watu wa taifa hilo kuweza kutoka na kuzalisha biashara zilizobora zaidi.
Balozi Chen, alisema Zanzibar, bado ina mazingira mazuri inayoweza kuyatumia kukuza uchumi wake pamoja na kuinua hali za wananchi hasa eneo la biashara.
Alisema vianzio vya utalii navyo ni vizuri pamoja na hali ya usaalama kuwa ni nzuri ambayo inaweza kukuza sekta ya uwekezaji.
Nae Waziri wa Mawasiliano na Miundombinu, Hamad Masoud, alisema serikali ya Zanzibar itaendelea kuuthamini mchango wa serikali ya China kutokana na misaada inayotoa kwa serikali.
Alisema Zanzibar kwa muda mrefu imekuwa ikifaidi mchango wa serikali ya China kutokana na kuwasaidia maktari ambao wameweza kuokoa maelfu ya Wazanzibari katika Hospitali za Unguja na Pemba.
Msaada mingine aliyeitaja ni pamoja na ujenzi wa jengo la soko la Mombasa, Nyumba za Mchina, jengo la Redio Zanzibar na kuwasomesha vijana wa Zanzibar na hivi sasa inajitayarisha kuisaidia Zanzibar katika kuweka mfumo mpya wa Digitali.
Alisema katika mafunzo hayo waliweza kujifunza zaidi katika makampuni makubwa 20 ambayo yameweza kuwaonesha njia bora.
Waziri huyo, alisema katika ziara hiyo Zanzibar itaweza kufaindika kupata wataalamu katika Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kwa kubadilishana wataalamu wa fani ya masomo ya kiswahili kuwafunza lugha hiyo nchini China.
No comments:
Post a Comment