Baadhi ya vipengele vyaondolewa
Na Mwantanga Ame
WAJUMBE wa Baraza la Wawakilishi walioanza kukutana jana kwa siku ya kwanza, kwenye mkutano wao wa wiki mbili, wameupitisha mswada wa mabadiliko ya sheria ya mafao ya viongozi wa Kitaifa.
Mabadiliko hayo yamefanywa ndani ya mswada wa mabadiliko ya sheria namba 4 ya mwaka 1988 na sheria ya viongozi wa kisiasa Namba 6 ya mwaka 1999, na kutunga sheria mpya ya maslahi na mafao ya viongozi wa kisiasa baada ya kustaafu na mambo yanayohusiana na hayo.
Mswada huo uliwasilishwa katika mkutano uliopita na kuchangiwa, ulipitishwa jana na wajumbe wa Baraza hilo baada ya serikali kuridhia kuvibadilisha na kuviondoa baadhi ya vipengele.
Awali akifanya majumuisho na kujibu hija za wajumbe wa Baraza hilo, waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Mwinyihaji Makame, alisema wameurejesha mswada huo baada ya wajumbe wa Baraza hilo kutaka kufanyiwa marekebisho kwenye baadhi ya vipengele.
Alisema serikali imeridhia mapendekezo ya wajumbe hao na kuviondoa vipengele vilivyoonekana kuleta utata ambapo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi amekubaliana na maoni ya wajumbe wa Baraza hilo.
“Serikali imeamua kuviondoa baadhi ya vipengele ambavyo wajumbe wa Baraza walipendekeza kuangaliwa upya”, alisema Mwinyihaji.
Dk. Mwinyihaji alisema vipengele hivyo vimerekebishwa na vyengine kuondolewa kutikana na usikivu alionao Rais kwa wajumbe wa Baraza hilo na ili sheria hiyo iweze kufanyakazi vizuri hapo baadae.
Alivitaja baadhi ya vipengele vilivyoondolewa ni pamoja na kile kinachowahusu malipo ya pencheni kwa watoto wa viongozi baada ya wazee wao kufariki, waliotajwa katika sheria hiyo.
Waziri huyo alisema kipengele chengine kilichoondolewa kinachohusu malipo kwa ajili ya washauri wa Rais ambapo sasa kwa vile Rais amepewa Mamlaka ya kuwaangalia viongozi hao atajua namna kuwatunza washauri hao.
Aidha, kipengele chengine kilichofanyiwa marekebisho ni kile kinachohusu juu ya kuwapatia ofisi Marais wastaafu baada ya kupatiwa kila mtu jengo la ofisi yake.
Alisema mswada huo hauna nia ya kuibebesha mzigo kama inavyodhaniwa kwani ilichokifanya kikubwa ni kuwawekea utaratibu utaoweza kuwaondolea matatizo viongozi hao utapofikia muda wa kustaafu.
Waziri huyo, alieleza serikali inawashukuru wajumbe wa Baraza hilo kwa kuridhia mabadiliko hayo baada ya Kiongozi wa Kamati ya Kusimamia Viongozi, inayoongozwa na Mwakilishi wa Jimbo la Kwamtipura Hamza Hassan Juma kukubaliana na mabadiliko hayo.
Baada hoja za waziri huyo, Baraza hilo lilipitisha sheria hiyo, huku Spika wake Pandu Ameir Kificho akiwashukuru kwa kuifanya kazi hiyo na kujali uzalendo kwa kuisaidia serikali.
No comments:
Post a Comment