Na Mwashamba Juma
SPIKA wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho amesema misaada inayotolewa na shirika la Mapango wa maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), limekuwa nguzo muhimu kwa Baraza hilo.
Spika Kificho alieleza hayo kwenye hafla fupi ya uzinduzi wa mradi wa kujengea uwezo vyombo vya kutunga sheria huko katika ukumbi wa hoteli ya Maruhubi Beach Villa, iliyoandaliwa na UNDP.
Alisema UNDP kwa kiasi kikubwa imesalisaidia Baraza lake katika kulijengea uwezo hali ambayo imechangia kukuwa kwa demokrasia nchini.
Akizungumzia mpango huo, Spika Kificho alisema kubuniwa kwake umejumuisha na kugusia maeneo muhimu katika demokrasia kwa vyombo vya kutunga sheria na hali hiyo imelisaidia Baraza la Wawakilishi kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
Aidha alitoa shukurani za dhati kwa shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa UNDP, kwa mashirikiano ya DFID, mfuko wa Umoja wa Mataifa na ubalozi wa Afrika Kusini kwa fanikisha mradi huo.
Nae Mwakilishi wa shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa UNDP, Philippe Poinsot alisema kuzinduliwa kwa mradi huo kutazidi kufanikisha urafiki uliopo baina ya Umoja wa Mataifa na serikali ya Zanzibar.
Alisema mradi umekuja muda muafaka ambapo Baraza linatekeleza majukumu yake mapya katika maisha ya Zanzibar ambapo taifa limo katika uongozi wa mfumo mpya wa serikali ya Umoja wa Kitaifa iliyofanikiwa kudhibiti amani ya kisiasa.
Alisema urafiki baina ya Zanzibar na shirika hilo ni kwa ajili ya maendeleo ya vyombo vya kutunga sheria ambavyo ni Baraza la Wawakilishi pamoja na Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
Aidha alisisitiza kuwa urafiki huo ni thamani kwa dunia kwasababu unaimarisha serikali za kidemokrasia kwa kusaidia nchi na jamii katika kuimarisha uongozi mzuri na demokrasia ya kweli kwa kuunda vyombo vya kutunga sheria vilivyo makini.
Kwa upande wake serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imesema kuwepo kwa Baraza la Wawakilishi lenye uwezo wa kutekeleza majukumu yake ipasavyo kwa mujibu wa katiba na sheria za nchi kutasaidia kwa kiasi kikubwa kujenga nchi yenye kufuata misingi ya uhuru, haki, udugu na maendeleo.
Akizungumza kwa niaba ya SMZ, Naibu Waziri wa Afya, Dk.Sira Ubwa Mamboya, alisema mradi huo utawasaidia wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuelewa vizuri majukumu yao kwa kuzingatia masharti ya katiba, sheria na kanuni za baraza.
Aidha alisema Serikali ipo tayari kushirikiana Shirika la UNDP na pia inaunga mkono jitihada zinazotolewa Shirika hilo si tu kwenye mradi huo bali na miradi mingine pia.
No comments:
Post a Comment