Habari za Punde

Mbarouk aonya watakaoibughudhi ZFA

Ataka wadau watoe ushirikiano kuendeleza soka

Na Abdi Shamnah

WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Said Ali Mbarouk, amewataka wadau wa michezo nchini, kukipa nafasi Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) kufanya shughuli zake bila bughudha, na kuonya kuwa hatawavumilia wale wanaolenga kukivuruga.

Akizungumza katika ufunguzi wa michuano ya soka ya Jimbo la Magogoni ‘Jihad Cup’ kwenye uwanja wa Welezo, Mbarouk amesema ni wajibu wa wadau wa soka nchini kukipa ushirikiano na kukiunga mkono chama hicho katika juhudi zake za kukuza soka badala ya kulenga kukidhoofisha
.

Alisema Wizara yake haitakuwa tayari kuona kunakuwepo watu wa aina hiyo kwani hawasaidii serikali katika azma yake ya kuendeleza michezo nchini, ikiwemo soka, zaidi ya kuibua migogoro.

Mbarouk alisema tayari uongozi wa wizara yake, umekubaliana kwa dhati na Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar (BTMZ) na ZFA, kufanya kazi ya kuimarisha soka na kukiachia jukumu chama hicho la kuandaa mikakati ili Zanzibar iweze kupata mafanikio katika kipindi kifupi kijacho.

Alisema wadau wote wanakaribishwa kutoa mawazo yao kwa mujibu wa sheria na kanuni za nchi, na aliwataka waelewe kuwa vyombo hivyo vipo kwa mujibu wa katiba.

Alizitaka klabu zote nchini kuviunga mkono vyombo hivyo, kwa kuzingatia umuhimu wa kuwepo mashirikiano kati ya wadau wote, kuanzia ngazi ya klabu hadi serikali.

Waziri huyo alimpongeza Mwakilishi wa Jimbo la Magogoni Abdillah Jihad Hassan kwa uamuzi wake wa kuanzisha michuano hiyo, na kusema itakuza ushirikiano na kuibua vipaji vya soka jimboni humo, huku akiwataka washiriki wa michuano hiyo kuzingatia suala la nidhamu na kuelewa kuwa michezo si ugomvi.

Aliahidi kuwa, ataizawadia shilingi laki moja timu yoyote itakayoibuka na ushindi wa nidhamu, wakati mshindi wa kwanza wa michauno hiyo, akiahidi kumtunuku shilingi 250,000 na mshindi wa pili shilingi 150,000.

Jumla ya timu tisa zinashiriki michuano hiyo zikiwa katika makundi mawili, ambazo ni Danger Boys, Sayari FC, Grenada, Maisara FC na Super Eagles, University, New Africa, Taifa jipya na Eleven Fighters.

Katika mchezo wa ufunguzi wa ngarambe hizo, timu ya Maisara ilianza vyema kwa kuitandika Grenada bao 1-0.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.