Na Faki Mjaka-Maelezo
Rais wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohammed Shein leo ameongoza Maelfu
ya wananchi na viongozi mbali mbali wa Serikali katika mazishi ya aliyekuwa
Brigedia Jenerali Msataafu Marehemu Adam Clement Mwakanjuki ambayo yamefanyika
Makaburi ya Mwanakwerekwe Zanzibar.
Mazishi hayo ambayo
yalifanyika kwa heshima zote za kijeshi kwa kupigwa mizinginga 11 baridi, yalihudhuriwa
pia na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani Dk.Gharib Bilal,Rais
Msaafu wa Zanzibar Aman Abeid Karume,na viongozi wengine wa ngazi za juu wa
Vyama vya siasa na Serikali.
Akitoa salamu za
Serikali mazishini hapo Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Mohammed
Aboud Mohammed amemuelezea marehemu Mwakanjuki kuwa alikuwa mtu muadilifu na
mwenye busara ambapo kifo chake kimetokea likiwa Taifa la Watanzani bado
linamuhitaji.
Waziri Aboud
amesema Marehemu Brigedia Jenerali Mstaafu alikuwa ni kiongozi Jemedari na
shupavu ambapo aliweza kulitumikia vyema Jeshi la Wananchi wa Tanzania kwa
uadilifu mkubwa jambo ambalo lilimjengea sifa hata katika siasa.
Amemuelezea
Brigedia Jenerali Mwakanjuki kuwa alikuwa ni kisima cha
ushauri,nasaha,maelekezo,busara siyo tu kwa masuala ya kisiasa na kijamii bali
pia masuala ya kiuchumi.
Marehemu alipata
Elimu yake ya msingi Skuli ya St.Paul Kiungani Zanzibar mwaka 1947-54 na
kujiunga na Elimu ya Sekondari ya St.Andrew ya Minaki jijini Dar es Salaam na
kupata Elimu ya Juu katika Chuo cha Fritz Heckert nchini Ujerumani ambapo alipata
masomo ya siasa 1960-1962
Mwaka 1964-1968
Marehemu aliajiriwa Idara ya Mambo ya nje ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kabla ya kujiunga na Jeshi la Wananchi wa Tanzania mwaka 1969.
Mwaka 1972-1979
alikuwa Mkuu wa Vikosi vya JWTZ na JKT ambapo mwaka 1980-1981 Brigedia Jenerali
Mwakanjuki alikuwa Kamisaa wa Divisheni ya 20 ya JWTZ.
Aidha Marehemu
alipata mafunzo mbali mbali ya uongozi katika Chuo cha Taifa cha Uongozi
Monduli na kupanda vyeo hadi mwaka 1988 alipopata cheo cha Brigedia Jenerali
hadi mwaka 1994 alipostaafu Jeshi.
Kabla ya kifo
chake Marehemu aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali za uongozi katika Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar zikiwemo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa
na Vikosi vya SMZ, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Katiba na Utawala Bora,Waziri
wa Kilimo,Mifugo na Mali Asili,Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi,Mjumbe wa
Baraza la Mapinduzi na Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar.
Marehemu amefariki
akiwa na umri wa miaka 73 ameacha Kizuka na watoto saba.
IMETOLEWA NA
IDARA YA HABARI MAELEZO ZANZIBAR
22/04/2012
No comments:
Post a Comment