Na
Abdi Shamnah
WAZIRI
wa Habari,Utamaduni,Utalii na Michezo, Said Ali Mbarouk amewataka wadau wa
michezo nchini, kukipa nafasi Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) kufanya shughuli
zake bila bughdha, na kuonya kutowavumilia wale wanaolenga kukivuruga.
Akizungumza
katika ufunguzi wa michuano ya soka Jimbo la Magogoni ‘Jihad Cup’ inayoendelea katika kiwanja cha
Welezo, Mbarouk amesema ni wajibu wa wadau wa soka nchini kukipa ushirikiano na
kukiunga mkono Chama hicho katika juhudi zake za kukuza soka badala ya kulenga
kukidhoofisha.
Alisema
Wizara yake haitakuwa tayari kuona kunakuwepo watu wa aina hiyo kwani
hawasaidii Serikali katika azma yake ya kuendeleza soka nchini, zaidi ya kuibua
migogoro.
Mbarouk
alisema tayari Uongozi wa Wizara yake, umekubaliana kwa dhati na BTMZ na ZFA
kufanya kazi ya kuimarisha soka na kukiachia jukumu chama hicho la kuandaa
mikakati ili Zanzibar iweze kupata mafanikio katika kipindi kifupi kijacho.
Alisema
wadau wote wanakaribishwa kutoa mawazo yao wa mujibu wa sheria na kanuni za
nchi na aliwataka waelewe kuwa vyombo hivyo vipo kwa mujibu wa Katiba.
Alivitaka
vilabu vyote nchini kuviunga mkono vyombo hivyo, kwa kuzingatia umuhimu wa
kuwepo mashirikiano kati ya wadau wote, kuanzia ngazi ya klabu hadi Serikali.
Akizungumzia
uanzishwaji wa Jihad Cup, Waziri Mbarouk alimpongeza Mwakilishi wa Jimbo la
Magogoni Abdillah Jihad kwa uamuzi wake wa kuanzisha michuano hiyo na kusema
itakuza ushirikiano na kuibua vipaji vya soka jimboni humo.
Aliwataka
washiriki wa michuano hiyo kuzingatia suala la nidhamu na kukubali matokeo ya
mchezo, kwa kigezo kuwa michezo sio ugomvi.
Akitilia
umuhimu wa hilo, Waziri Mbarouk aliahidi kuitunuku shilingi 100,000/- timu yoyote
itakayoibuka na ushindi wa nidhamu, wakati ambapo mshindi wa kwanza wa michauno
hiyo kuahidi kumzawadia 250,000/- na mshindi wa pili shilingi 150,000/-.
Nae
Makamu wa Rais ZFA, Al Haji Ameir , alisema michuano hiyo inafanyika kulingana
na kalenda ya ZFA , inayoainisha kuwepo kwa mashindano ya majimbo, hivyo
aliwataka wachezaji wanaoshiriki kujituma, kwa kigezo kuwa makocha wa ZFA wa
U.15, U.17 na U.20 watafika kutafuta vipaji.
Jumla
ya timu tisa zilizo katika makundi mawili zinashiriki katika michuano hiyo,
ambazo ni Danger boys,Sayari FC, Grenada, Maisara FC na Supper Eagles.Nyengine
ni University,New Africa,Taifa jipya na Eleven fighter.
Mshindi
wa kwanza wa michuano hiyo atazawadi Kombe,Jezi seti moja,mipira mitatu na sh.150,000/
wakati mshindi wa pili ataondoka na jezi seti moja,mipira miwili na sh.100,000/
na mshindi wa tatu atapata jezi seti moja, mipira miwili na sh.50,000/.
Katika
pambano la fungua dimba timu ya Maisara ilianza vizuri michuano hiyo kwa
kuondoka na ushindi baada ya kuibamiza Grenada kwa bao 1-0.
No comments:
Post a Comment