Na Madina Issa
TATIZO la migogoro ya ardhi iliyoibuka Zanzibar bado inaendelea kushamiri katika vijiji mbali mbali, baada ya kudaiwa kuibuka kwa mgogoro mwengine katika shehia ya Kizimkazi Dimbani Wilaya ya Kusini Unguja.
Mgogoro huo ambao kwa sasa umeingia hatua ya kuwahusisha wenyewe kwa wenyewe unahitaji jitihada za makusudi kuutatuwa haraka na vyombo vinavyosimamia ardhi, ili kuweza kuepusha madhara makubwa yanayoweza kutokea hapo baadae.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Kijijini kwao Kizimkazi Dimbani Wilaya ya Kusini Unguja, Kaimu Mwenyekiti wa kamati ya Maendeleo Kijijini hapo, Hamid Abdulhamidi Khamis alisema licha ya juhudi zinazochukuliwa kudhibiti maeneo hayo, hali imezidi kuwa mbaya zaidi kutokana na baadhi ya wananchi ndani ya kijiji hicho kuwa chanzo cha mgogoro.
Alisema kamati hiyo inafanya kazi ya kugawa viwanja baada ya kupewa idhini na idara ya ardhi kisheria, kusimamia kikamilifu maeneo hayo, na kuyagawa kwa kufuata mwongozo wa ardhi wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Jumla ya viwanja 356 vinatarajiwa kugawiwa kwa wananchi hao katika mji Mpya wa Kizimkazi Dimbani,
“Sisi kama ni wasimamizi wa eneo hili hatujagawana viwanja sehemu za mbele isipokuwa kila aliyekuja mwanzo tunampa nafasi hiyo kwa wakati waliokuja”alifahamisha Kaimu Mwenyekiti huyo.
Nae Diwani mstaafu Wadi ya Kizimkazi, Abdulaziz Hamad Ibrahim, alisema matatizo ya Ardhi yaliyoibuka katika shehia hiyo hawatoweza kuyamalizika kwani hivi sasa kumejitokeza baadhi ya watendaji wa Serikali ngazi ya Wilaya na Shehia ikiwa wataendelea kuchukuwa rushwa na kujali maslahi binafsi na kuwaacha wananchi wakiwa wanalalamika.
Alisema kuwa hivi sasa nguvu za ziada zinahitajika kati ya viongozi wa Mkoa na Serikali kuu kumaliza matatizo hayo ya ardhi ambayo yanaitia sura mbaya katika Kijiji chao.
Alisema kuwa hivi sasa uongozi wa Wilaya hawajakutana na Kamati hiyo lakini invyoonekana wanafanya vikao vyao binafsi huku wakichukua Rushwa na ndio maana hawataki kukutana na viongozi wa kamati hiyo.
“sisi ushahidi tunao kwa watu wa Wilaya hiyo kuwa wanachukua rushwa na ushahidi tunao na mukiutaka tutawapa mbele ya hata viongozi wa juu”alisema Ibrahim.
Hata hivyo kamati hiyo imeutaka Uongozi wa Wilaya pamoja na shehia kufuata maadili ya kazi zao na kuachana na tabia ya kutumia madaraka yao kwa maslahi yao binafsi.
Nae sheha wa shehia hiyo Abdulrazak Hassan Ibrahim kwa upande wake alisema kuwa yeye hashirikishwi kikamilifu katika vikao vya kamati hiyo wanavyoviamua na ndiko kunakochangia kuongezeka migogoro katika maeneo hayo ya Mchangamle na mji mpya kutokuwa na uwamuzi wa upande mmoja.
Alifahamisha kuwa hivi sasa tayari lipo agizo kutoka Wilaya ya Kusini juu ya kusimamisha zoezi linalofanywa na kamati ya ugawaji wa viwanja lakini pia limepuuzwa na kamati.
Nae Afisa Wilaya ya Kusini, Abdallah Ali Kombo, alikiri kuwepo kwa migogoro hiyo na hivi sasa wapo kulitatua suala hilo kwa kusema kuwa wamewaita kamati hiyo lakini hawajaja.
“Sisi kama Wilaya tumewaita lakini kamati hiyo haijaja na wala hawajatwambia lolote na hadi hivi sasa hawajaja kusikiliza”alifahamisha ofisa huyo.
Hata hivyo alisema kuwa kamati hiyo ipo kwa kundi maalum na sio kuwahudumia wananchi wa Kijiji hicho kwani hivi ssasa kumejitokeza kamati hiyo kuviuza viwanja vilivyokuepo kwenye mji Mpya.
Hivyo alitoa wito wa wananchi wa Kizimkazi kuwa na moyo wa subira kwa tatizo hilo kwani Wilaya imo katika kulitatua tatizo hilo kwani Wilaya ipo kwa wananchi wote bila ya kjali Dini, Rangi, wala Chama.
No comments:
Post a Comment